• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Ruto avuna wafuasi eneo la Magharibi

Ruto avuna wafuasi eneo la Magharibi

NA SHABAN MAKOKHA

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu Rais William Ruto kinazidi kujizolea umaarufu katika Kaunti ya Kakamega.

Chama hicho kimeendelea kuvuna wanachama kutoka vyama vya muungano wa Kenya Kwanza na Azimio la Umoja siku chache tu kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Vyama vya Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) na Amani National Congress (ANC), ndivyo wahasiriwa wa hivi punde baada ya kupoteza takriban wanachama 500 kwa UDA katika eneobunge la Mumias Mashariki.

Wanachama wasiopungua 350 wa DAP-K na 150 kutoka ANC, wamehama vyama vyao ili kumuunga mkono mwaniaji wa UDA, Bw Benson Mapwoni wa Mumias Mashariki.

Katika eneo la Mumias Magharibi, zaidi ya wafuasi 500 wa Orange Democratic Movement (ODM), wamebadilisha msimamo wao kutoka kwa Bw Johnson Naicca na kuanza kumpigia debe Bw Rashid Echesa wa UDA.

Haya yamejiri huku kukiwa na hofu ya wagombea kutemwa katika jaribio la mwisho katika kambi za Raila Odinga na Dkt Ruto, la kupata idadi kubwa ya viti kwenye chaguzi za Agosti 9.

Bw Justin Malala, aliyedai kuwa mwenyekiti wa DAP-K Mumias Mashariki na aliyewaongoza wanachama kutema chama hicho, alisema walichukua uamuzi huo, baada ya mgombea wao wa ubunge Peter Kalerwa (PK) Salasya, kuwatoroka na kuhamia mjini Bungoma alipopatiwa gari na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa.

“Bw Wamalwa alitaka kumsaidia alipompatia gari na dereva ili kurahisisha safari zake wakati wa kampeni. Bw Salasya anatumia vibaya fursa hiyo kwa burudani. Tunahitaji mgombea aliyejitolea atakayetuongoza kupata ushindi,” alidai Bw Malala.

Aidha, alimshutumu mwaniaji huyo wa DAP-K kwa kuingiwa na kiburi na ukaidi baada ya maisha yake kuboreshwa na Bw Wamalwa.

“Tukimruhusu ashinde uchaguzi tutalaumiwa na wapigakura wa Mumias Mashariki kwa sababu hana sifa za kiongozi halisi. Hatuwezi kuwa tunamfanyia kampeni mashinani akiwa amelala mjini Bungoma,” alisema.

Hisia zake zilipuuziliwa mbali na Bw Mathews Namatsi, aliyedai kuwa mwenyekiti rasmi akisema wanaodai kuhama chama hicho ni matapeli.

“Hakuna mwanachama wetu ameondoka. Tumepitia sajili yetu na majina yao hayapo kwenye orodha ya wanachama wetu,” alisema Bw Namatsi.

Bw Namatsi alisema wanachama wote wa DAP-K Mumias Mashariki wanamuunga mkono kikamilifu Bw Salasya huku akiwahimiza wapigakura wasiyumbishwe na propaganda.

Bw Salasya alimshutumu vikali mbunge anayeondoka Benjamin Washiali akimlaumu kwa kusambaza propaganda ili kumfanya mgombea wake, Bw Mapwoni, aonekane kama anayeongoza katika kinyang’anyiro cha ubunge.

“Kataeni njama za Washiali kupitia Mapwoni ili tuchunguze jinsi amesimamia fedha za eneobunge. Kwa muda wa miaka mitatu, hatujakuwa na msimamizi thabiti wa Fedha katika eneobunge la Mumias Mashariki na hili linaibua shaka kuhusu matumizi ya fedha za ugatuzi katika eneobunge hili,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Lugogo afurahia kurudi Bandari akitokea Sofapaka

Serikali kutoa dawa za minyoo kwa watoto milioni 6

T L