• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Serikali kutoa dawa za minyoo kwa watoto milioni 6

Serikali kutoa dawa za minyoo kwa watoto milioni 6

NA KENYA NEWS AGENCY

SERIKALI imeanzisha mpango maalum unaolenga kuwapa watoto milioni sita kote nchini dawa za kuangamiza minyoo.

Mradi huo wa Kitaifa unadhamiriwa kunufaisha watoto wenye umri kati ya miaka 2-14 katika kaunti zote nchini.

Kaunti ya Busia inaongoza huku jumla ya watoto 297,000 wenye umri wa chini ya miaka 14 wakitazamiwa kupatiwa dawa hizo.

Mradi huo Kuangamiza Minyoo Shuleni (NSBDP), utatoa matibabu katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na aina mbili ya maambukizi yanayosababishwa na minyoo kupitia mchanga.

Maambukizi hayo ni miongoni mwa maradhi yaliyotelekezwa na yanayoathiri afya ya watoto na elimu.

NSBDP imekuwa ikisambaza dawa za kuangamiza minyoo kwa watoto shuleni kupitia awamu tisa za matibabu kufikia sasa.

Akizungumza Jumapili katika hafla ya kuadhimisha miaka kumi ya NSBDP, Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya, Dkt Rashid Aman, alisema watoto wote wenye umri wa chini ya miaka 14 watapatiwa dawa za minyoo na walimu shuleni bila kujali hadhi yao.

Hafla hiyo iliyofanyika katika Shule ya Msingi ya Mundika Boys, Kaunti ya Busia, iliandaliwa na Wizara za Afya na ile ya Elimu pamoja na shirika la Evidence Action.

“Busia ni kituo cha utafiti maarufu uliofahamisha miradi ya kimataifa na ya humu nchini kuhusu manufaa ya kuwapa dawa za minyoo watoto waliohitimu umri wa kwenda shule. Minyoo wanaopatikana kwenye utumbo ni tatizo kuu la afya ya umma nchini Kenya. Watoto zaidi ya milioni sita wanakabiliwa na tishio la maambukizi kila mwaka. Maambukizi ya minyoo husababisha utapiamlo licha ya kupata lishe bora,” alisema Waziri Aman.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu wa Wizara ya Elimu, Bw Andrew Lukalia alisema matibabu yanayoendeshwa shuleni yanawalinda mamilioni ya watoto Wakenya dhidi ya minyoo na kuwapa manufaa tele kiafya.

Afisa huyo alisema lishe bora kwa watoto inatoa msingi kwa watoto kujifunza, kustawi na kukua kama watu wazima wenye afya.

Kote duniani, watoto karibu milioni 900 wanakabiliwa na tishio la kuambukizwa na minyoo wanaosambazwa kupitia mchanga almaarufu helminths (STH), huku wengi wakiwa hatarini kuambukizwa schistosomiasis vilevile.

  • Tags

You can share this post!

Ruto avuna wafuasi eneo la Magharibi

Wawaniaji walilia IEBC wakidai serikali ya Joho...

T L