• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Ruto awaahidi kinamama vinono akiunda serikali

Ruto awaahidi kinamama vinono akiunda serikali

NA MARY WANGARI

NAIBU wa Rais William Ruto jana Ijumaa aliahidi vinono wanawake katika serikali yake iwapo atashinda urais Agosti 9.

Dkt Ruto alitia saini mkataba wa maelewano na wanawake katika juhudi za kujaribu kuzima wimbi la umaarufu wa mwaniaji mwenza wa Azimio, Martha Karua ambaye anaonekana kuwa kivutio kwa kina mama.

Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, umaarufu wa mwaniaji wa urais wa Azimio, Raila Odinga umeongezeka tangu alipomteua Bi Karua kuwa mgombea mwenza wake.

Katika hafla iliyojaa mbwembwe uwanjani Nyayo, Nairobi, Naibu Rais alitoa ahadi tele ikiwemo kuwatengea nyadhifa serikalini, kuboresha afya na kuwakweza kiuchumi ikishinda urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Katika mkataba huo, Dkt Ruto aliahidi kuwatengea wanawake asilimia 50 ya viti vya uwaziri.

Hiyo inamaanisha kuwa vinara wenza wakuu wa Kenya Kwanza Mabw Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya) ambao wameahidiwa nafasi sita za uwaziri, watalazimika kupendekeza majina ya wanawake watatu.

Ruto alitangaza kuwahusisha rasmi viongozi wanawake katika vikosi vinavyomsaidia kusaka kura katika maeneo mbalimbali nchini.

Aliahidi kuwa serikali ya Kenya Kwanza itahakikisha inapitisha sheria ya kuhakikisha kunakuwa na angalau theluthi moja ya wanawake Bungeni na idara mbalimbali serikalini.

Alisema mswada huo utapitishwa ndani ya siku 90 baada ya kuapishwa kwake kumrithi Rais Kenyatta.

Ahadi hiyo, hata hivyo, huenda isitekelezwe ndani ya muda uliowekwa haswa ikizingatiwa kuwa mswada wa usawa wa jinsi umetupwa mara nne tangu kuanza kutekelezwa kwa Katiba ya 2010.

Wengi wa wabunge wanaume wamekuwa wakikosa kwenda Bungeni hivyo kusababisha mswada kutupwa kwa kukosa idadi inayohitajika kupigia kura mswada.

Naibu wa Rais atahitaji kuwa na idadi kubwa ya wabunge kumwezesha kupitisha mswada huo haraka.

Aidha, aliahidi kuanzisha kitengo maalum katika Afisi ya Rais, kitakachoshughulikia haki za wanawake pamoja na kuwapa usemi kuhusu mali ya ndoa.

Kitengo hiki kitashughulikia matatizo yote yanayowakumba wanawake kuanzia ukeketaji, dhuluma za kingono, unyanyasaji nyumbani kati ya masuala mengineyo.

Kuhusu afya, Kenya Kwanza imeahidi kuhakikisha wanawake wote wamesajiliwa na NHIF huku ikiahidi kuwapa kina mama nepi za watoti miezi mitatu ya kwanza baada ya kujifungua.

Alisema serikali yake itatenga Sh25 bilioni kwa ajili ya kuinua biashara za akina mama.

Naibu wa Rais alisema kuwa atabuni mpango wa ‘Rejea Shule’ unaolenga kuhakikisha kuwa wasichana wanaopachikwa mimba za mapema wanaendelea na masomo yao baada ya kujifungua.

Wanafunzi na wanawake maskini watakuwa wanapewa sodo za bure baada ya serikali ya Kenya Kwanza kuchukua hatamu za uongozi.

  • Tags

You can share this post!

Raila atuma Karua ngome ya Ruto

Wakazi wa Gatundu wapokea miche ya macadamia

T L