• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Ruto na Raila washikilia misimamo mikali

Ruto na Raila washikilia misimamo mikali

NA CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa Kenya Kwanza na Azimio la Umoja-One Kenya mnamo Ijumaa waliendelea kuchukua misimamo mikali licha ya viongozi wa kidini kuwataka Rais William Ruto na Raila Odinga kufufua mazungumzo kuzuia maandamano yanayosababisha maafa na uharibifu wa mali.

Mnamo Ijumaa, Rais Ruto aliapa kuwa maandamano hayatafanyika Jumatano wiki ijayo huku akionya kukabiliana “vikali” na Bw Odinga. Lakini uongozi wa Azimio ulijibu kwa kutangaza kuwa maandamano ya kupinga serikali sasa yatafanyika siku tatu mfululizo; kuanzia Jumatano hadi Ijumaa kuanzia wiki ijayo.

“Hayo maandamano hayatafanyika tena. Nisikilize kwa makini. Hauwezi kutumia mbinu haramu na zinazokiuka Katiba kusaka mamlaka Kenya. Subiri hadi 2027 na nitakubwaga tena,” Rais Ruto akasema Ijumaa akionekana kumrejelea Bw Odinga.

“Uchaguzi umekamilika. Hauwezi kusaka uongozi kwa kutumia damu ya Wakenya pamoja na kuharibu mali ya umma,” akaongeza alipokuwa akiwahutubia wananchi baada ya kufungua barabara ya Naivasha-Njabini.

Rais Ruto pia alikariri kuwa, hatafanya handisheki na Bw Odinga akisema hiyo ndio chanzo cha matatizo yanayoizonga Kenya wakati huu kama vile mzigo wa madeni na kupanda kwa gharama ya maisha.

“Nitasimama imara. Sitatikisika. Kenya ni yetu sote; sio ya waandamanaji. Fanya maandamano nyumbani kwako sio mahala popote nchini,” akasema Dkt Ruto.

Kwa upande wake, Naibu Rais Rigathi Gachagua alishutumu Bw Odinga akimtaja kama “Mzee mwenye umri wa miaka 80 ambaye hawezi kutoa suluhu kwa matatizo yanayowakumba Wakenya. “Hii ndio maana Wakenya walikukataa kwa mara ya tano katika uchaguzi mkuu uliopita,” akasema.

Sawa na bosi wake, Bw Gachagua alipuuzilia mbali miito ya viongozi wa kidini kwamba waridhiane kisiasa na Bw Odinga.

“Serikali haitakubali vitisho. Wale wanaosema kuwa Rais azungumze na yule jamaa hawajui wanachosema. Rais wetu hana muda huo; amebanwa na shughuli za kuwahudumia Wakenya,” akasema.

Lakini muda mfupi baada Rais Ruto na Bw Gachagua kutoa kauli hizo kali, uongozi wa Azimio ulitangaza kuwa, maandamano sasa yatafanyika siku tatu mfululuzo kila wiki kuanzia Jumatatu ijayo “kutokana na shinikizo kutoka kwa umma.”

“Kuanzia sasa, maandamano ya amani kote nchini yatafanyika Jumatano, Alhamisi na Ijumaa kuanzia juma lijalo. Tumefikia uamuzi huu baada ya kupokea maombi kadhaa kutoka kwa wananchi,” ikasema taarifa ya Azimio iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Mnamo Alhamisi, Bw Odinga alisema maandamano hayo, ambayo yamechangia maafa na uharibifu mkubwa wa mali, yatarejelewa Jumatano wiki ijayo.

“Tutarejelea maandamano yetu Jumatano baada ya muda wa siku tano ambao tutautumia kuomboleza Wakenya waliouawa Jumatano kikatili na polisi,” Bw Odinga akasema kwenye kikao na wanahabari katika afisi za Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga (JOOF), Nairobi.

Huku hayo yakijiri, viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu walitoa wito kwa Rais Ruto na Bw Odinga kupatana ili kuzuia maandamano.

Kiongozi wa Baraza la Makanisa Nchini (NCCK) Askofu Mkuu Timothy Ndambuki na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini (KCCB) Askofu Mkuu Martin Kivuva walimtaka Rais Ruto “kuwahurumia Wakenya ambao wanakabiliwa na makali ya kupanda kwa gharama ya maisha na ukame.”

Viongozi hao walimtaka Rais kusitisha utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya 2023 ili kuondoa mzigo wa ushuru kwa Wakenya.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu Nchini (SUPKEM) tawi la Rift Valley Sheikh Abubakar Bini pia alitoa wito kwa maridhiano kati ya Rais Ruto na Bw Odinga

Isitoshe, Ijumaa, Msemaji wa Afisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kibinadamu Jeremy Laurence alipendekeza uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu vifo na majeruhi yaliyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya Jumatano.

“Aidha, tunatoa wito kwa maafisa wa usalama kuhakikisha usalama kwa waandamanaji wiki ijayo kwani maandamano yanaruhusiwa na Katiba ya Kenya pamoja na Sheria za Kimataifa,” akasema kwenye taarifa.

  • Tags

You can share this post!

Makahaba wa mijini wakubali mavuno ya shambani,...

Haji ni fuko wa Raila?

T L