• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Haji ni fuko wa Raila?

Haji ni fuko wa Raila?

NA MWANGI MUIRURI

MWEZI mmoja tu baada ya Mkurugenzi wa Idara ya Ujasusi nchini (NIS) Noordin Haji kuapishwa, baadhi ya wanasiasa wa muungano tawala wa Kenya Kwanza sasa wanamshuku kuwa fuko wa upinzani.

Bw Haji aliapishwa mnamo Juni 14, 2023 kuchukua hatamu za NIS kurithi mikoba ya Wachira Kameru.

Baadhi ya wanasiasa waliohudhuria Mkutano wa Muungano huo katika Ikulu ya Nairobi mnamo Julai 15, 2023 walimnyooshea kidole cha lawama kwa kile walikitaja ni kuwa na msimamo wa kupendelea kinara wa upinzani Bw Raila Odinga.

Aidha, anatuhumiwa kupendelea maelewano yawepo baina ya Bw Odinga na Rais William Ruto.

Isitoshe, ukuruba wake na Rais mstaafu Bw Uhuru Kenyatta pia umejadiliwa.

“Ni vyema ieleweke kuwa Bw Haji huwa anaonekana alikutana na Bw Odinga na Bw Kenyatta. Anafaa aamue kama yeye ni mwanasiasa wa Azimio ama yeye ni mfanyakazi wa umma,” akasema mmoja wa viongozi hao katika mkutano wa Ikulu.

Taifa Leo ilifichuliwa kwamba baadhi ya viongozi hao walipendekeza Bw Haji azomewe katika Bunge la Kitaifa na Seneti na ikihitajika, ang’olewe.

Baadhi ya viongozi hao waliteta kwamba NIS imekuwa na uzembe mwingi kiasi kwamba katika siku za maandamano, magenge huchipuka bila idara hiyo kujua hivyo basi kuifanya kazi ya polisi kuyazima kuwa ngumu.

Katika hali hiyo, vinara wa walio wengi katika Bunge la Kitaifa na Seneti Mbw Kimani Ichung’wa na Aaron Cheruiyot mtawalia, walitoa taarifa kwa vyombo vya habari wakisema watakuwa wakikabiliana na wakereketwa wa maandamano.

Kupitia taarifa ya pamoja, wawili hao walisema kwamba kuanzia Jumatano ijayo ambapo wakereketwa hao wametangaza kushiriki maandamano, “tutajitokeza kama viongozi, wafuasi wa serikali na wengine kushirikiana na vyombo vya kiusalama kulinda maisha ya raia, biashara, nchi na demokrasia yetu”.

  • Tags

You can share this post!

Ruto na Raila washikilia misimamo mikali

Vitisho vya viongozi na wandani vyaweka raia pabaya

T L