• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 2:33 PM
Ruto, Raila walenga kudhibiti mabunge

Ruto, Raila walenga kudhibiti mabunge

NA CHARLES WASONGA

WAGOMBEAJI wakuu wa urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, Naibu Rais William Ruto (UDA) na Bw Raila Odinga (Azimio), wanang’ang’ania kudhibiti bunge la kitaifa na seneti kwa kuweka mikakati itakayowezesha mirengo yao kushinda viti vingi katika mabunge hayo.

Hii, kila moja mmoja anaamini, itamwezesha kufanikisha utekelezaji wa ahadi nyingi ambazo ametoa katika kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Ili kufikia lengo hilo, Azimio inawashawishi wagombeaji wa viti hivyo wasio maarufu wajiondoe kuwapisha wenye ufuasi mkubwa, hasa katika ngome zake.

Muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Dkt Ruto pia unatumia mbinu hiyo hiyo ili kushinda viti vingi.

Mirengo hiyo miwili inataka kuhakikisha inashinda viti vingi vya ugavana na udiwani iweze kudhibiti idadi kubwa ya serikali za kaunti baada ya Agosti 9.

Wakuu wa Azimio waliambia Taifa Leo kwamba, hii ndio ilikuwa ajenda kuu ya mkutano wa Baraza Kuu la Azimio uliofanyika jana katika jumba la KICC, Nairobi.

“Hatutaki kukumbwa na hali ambapo tunashinda urais lakini tunakosea kwa kupoteza viti vingine kama vile ubunge, useneta na ugavana, haswa katika ngome zetu. Hii ndio maana mkutano wa leo (Ijumaa) umeamua wagombeaji mbalimbali waondolewe ili tushinde viti vingi bungeni,” Katibu Mkuu wa Azimio Junet Mohamed akasema baada ya mkutano huo ulioongozwa na Bw Odinga.

Vyama tanzu katika Azimio ndivyo vitatekeleza uamuzi huo kwa kuwashauri “wagombeaji dhaifu” wajiondoe katika uchaguzi. Hii itatoa nafasi kwa wagombeaji “wenye nguvu” kupambana na washindani kutoka mrengo wa Kenya Kwanza na wale wanaojitegemea.

Mkakati huu utatekelezwa katika maeneo ambako muungano wa Azimio una ushawishi mkubwa lakini unahisi kukabiliwa na upinzani mkubwa kutoka Kenya Kwanza na wagombeaji huru.

Maeneo hayo ni kama vile; Nairobi, Ukambani, Pwani, uliokuwa mkoa wa Magharibi, eneo la Gusii, Narok, Kajiado, Mlima Kenya na Kaskazini Mashariki.

“Wagombeaji viti mbalimbali kupitia vyama tanzu ndani ya Azimio kutoka maeneo haya wataathirika na uamuzi huu ambao japo mchungu, unafaa. Hamna maana kwetu kushinda urais bila wabunge na maseneta wengi watakaopitisha ajenda za Azimio,” akasema Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambaye ni mwanachama wa Baraza Kuu la Kitaifa la Azimio (NEC).

“Watakaojiondoa watatunukiwa nyadhifa zingine serikalini Raila akishinda. Kwa sasa hatutaki kugawanya kura zetu na kufaidi wapinzani wetu,” akaongeza.

Wadadisi wanasema kuwa wawaniaji wa viti vya ubunge kwa tiketi ya vyama vya Azimio katika kaunti ya Nairobi ndio wataathirika zaidi.

Kwa mfano, katika eneo bunge la Makadara vyama tanzu vya Azimio vimedhamini; George Aladwa (ODM), Mark Ndungu (Jubilee) na Fred Oketch (Wiper) watakaopambana na Anthony Waithaka wa United Democratic Alliance (UDA).

  • Tags

You can share this post!

Wataalam sasa wataka wanafunzi wa umri wa miaka 15 kupatiwa...

NYOTA WA WIKI: Victor Osimhen

T L