• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:47 AM
Sekta ya kilimo imepuuzwa – Ruto

Sekta ya kilimo imepuuzwa – Ruto

NA SAMMY WAWERU

GHARAMA ya juu ya chakula nchini inayoshuhudiwa imechangiwa kwa kiwango kikubwa na kupuuzwa kwa sekta ya kilimo.

Naibu wa Rais, Dkt William Ruto anayewania urais kupitia muungano wa Kenya Kwanza amesema kuendelea kupanda kwa bei ya bidhaa za kula kunatokana na “serikali kutojali sekta ya kilimo ambayo ni nguzo kuu katika ukuaji wa uchumi”.

Dkt Ruto amesema hayo Jumanne wakati wa mdahalo wa wagombea wa kiti cha urais unaoendelea, katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA).

“Tumenyima sekta ya kilimo mgao unaofaa… Tumeipokonya sekta hiyo ‘msaada’ inaopaswa kupata,” Dkt Ruto amesema.

Kiongozi huyo wa United Democratic Party (UDA), mojawapo ya chama kinachounda mrengo wa Kenya Kwanza, amedai kuendelea kufumbiwa macho kwa kilimo kumechochea pakiti ya unga wa mahindi kugonga Sh230.

Amesema bei hiyo ni ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini, hasa kipindi ambacho gharama ya maisha inaendelea kuwa ghali.

Serikali hata hivyo imezindua mgao wa bajeti ya muda kuishusha, hadi Sh100.

Tangazo hilo lilitolewa na Waziri wa Kilimo, Peter Munya siku kadha zilizopita, Rais Uhuru Kenyatta majuzi akitia muhuri mpango huo.

Kauli ya Dkt Ruto imeonekana kuwa kinaya – ‘kudai serikali imepuuza sekta ya kilimo’, katika serikali ambayo binafsi anashiriki kama naibu wa rais.

Akiuza sera kusaka kura kuwa rais wa tano wa Kenya kwenye mikutano ya kisiasa maeneo mbalimbali nchini, naibu rais amekuwa akisifia utendakazi wake wakati akiwa Waziri wa Kilimo, chini ya utawala wa serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki (ambaye kwa sasa ni marehemu) na kiongozi wa ODM, Raila Odinga kama Waziri Mkuu.

Ruto aidha amekuwa akihoji alisaidia kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo.

Amekuwa akilalamikia kutengwa katika maamuzi ya serikali, baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kutangaza kuzika tofauti zao za kisiasa kupitia mapatano ya Handisheki.

  • Tags

You can share this post!

Auawa kwa sababu ya mlo wa omena

Dereva ashtakiwa kwa kuiba sukari ya Sh3.2 milioni

T L