• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Serikali yaonya Raila kuhusu maandamano

Serikali yaonya Raila kuhusu maandamano

NA WAANDISHI WETU

SERIKALI imetoa onyo kali kwa viongozi wa upinzani na wafuasi wao kwamba, watakamatwa na kushtakiwa kwa kusababisha maafa na uharibifu wa mali katika msururu wa maandamano yaliyopigwa marufuku.

Tayari, watu 312 wamekamatwa kuhusiana na maandamano ya Jumatano, akiwemo Mbunge wa Mavoko Patrick Makau.

Rais William Ruto jana Alhamisi alikariri kuwa “nitamkalia ngumu” kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga kwa kutumia vijana kusababisha machafuko nchini.

“Nasema hapa kwamba, nitamkalia ngumu huyo mtu (Raila) ili aache kutumia vijana wetu kuharibu mali. Alimhangaisha Uhuru hadi mpango wetu wa Ajenda Nne za Maendeleo ukaharibika. Sasa asidhani kuwa atatumia maandamano kuvuruga mipango yetu ya kuwapa vijana hawa ajira,” akasema akiwa kaunti ya Tharaka Nithi.

Rais Ruto pia aliapa kumkabili Bw Odinga na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, kwa madai ya kufadhili ghasia nchini.

Nao Naibu Rais Rigathi Gachagua na mawaziri Musalia Mudavadi (Mkuu wa Mawaziri), Kithure Kindiki (Usalama), Kipchumba Murkomen (Uchukuzi) na Moses Kuria walisema serikali katu haitamruhusu kiongozi wa Bw Odinga na wafuasi wake kuharibu mali ya umma kwa kisingizio cha kupigania gharama ya maisha kushushwa.

Hii ni kufuatia ghasia zilizoshuhudiwa Jumatano wakati wa makabiliano kati ya maafisa wa polisi na waandamanaji katika miji kadhaa nchini ambapo watu saba waliuawa na mali ya mabilioni ya fedha kuharibiwa.

“Serikali imefikia kikomo na sasa itachukua hatua kali kabisa dhidi ya magenge hayo ya wahalifu. Hatutaruhusu hao watu wa Azimio kuwaua Wakenya kila mara, kuharibu mali ya umma na kuvuruga biashara za watu wetu,” Bw Gachagua akasema.

Naibu Rais alidai vijana waliopora mali katika eneo la Mlolongo na Kitengela ni wafuasi wa kundi haramu la Mungiki.

“Serikali itapambana na hawa pamoja na wadhamini wao, tunaowajua, bila huruma,” akaonya alipoongoza mradi wa ustawishaji sekta ya ufugaji, Laikipia. Kwa upande wake, Bw Mudavadi alifananisha ghasia zilizoshuhudiwa kwenyemaandamano ya Azimio na uhaini na njama ya kuporomosha nchi kiuchumi.

“Ghasia za Azimio ni uhaini kwa sababu zinalenga kuvuruga uchumi. Kama serikali, hatuwezi kukaaa kitako huku tukitizama mtu akiharibu kile ambacho taifa hili limejenga kwa miaka mingi ili kufanikisha matakwa yake ya kibinafsi,” akasema Bw Mudavadi akiwa eneo la Diani, kaunti ya Kwale.

Mkuu huyo wa Mawaziri alidai kuwa, serikali inapoteza Sh650 milioni kila siku, Sh20 bilioni kila mwezi na huenda ikapoteza Sh234 bilioni kwa mwaka kupitia maandamano.

“Hii ni hasara kwa mlipa ushuru. Sharti watu hawa wakamatwe na washtakiwe,” Bw Mudavadi akasema kwa hasira.

Naye Profesa Kindiki aliwaagiza maafisa wa polisi kukabiliana vikali na bila huruma na waandamanaji ambao aliwataja kama “magaidi.”

“Nawataka polisi wetu kuwa imara. Msicheze na wahalifu. Mpambane vikali na wahalifu hawa bila huruma. Kwa upande wetu, tutapambana na mtu yeyote atakayezuia maafisa wetu kufanya kazi yao,” akasema alipoongoza hafla ya ufunguzi wa kituo cha polisi katika eneo la Kiserian, kaunti ya Kajiado. Kwa upande wake, Bw Murkomen aliwahakikishia maafisa wa polisi kwamba, serikali inawaunga mkono asilimia 100 katika juhudi zao za kutibua maandamano ya Azimio.

Akiongea alipokagua uharibifu katika barabara ya Nairobi Express Way, Bw Murkomen alisema serikali itakamata wote waliohusika na uharibifu huo.

“Waliobomoa vyuma vya barabara hii na kuteketeza mali hawatasazwa. Watakamatwa na kulasimishwa kugharamia hasara hii ya kima cha Sh700 milioni,” akafoka huku akiandamana na maafisa wa usalama.

Bila kutoa ithibati yoyote, Waziri wa Biashara Moses Kuria alidai kuwa fujo zilizoshuhudiwa katika eneo la Mlolongo wakati wa maandamano ya Jumatano zilisababishwa na maskwota haramu katika shamba la kampuni ya saruji ya East Africa Portland.

“Chanzo cha ghasia na uharibifu wa mali katika eneo la Mlolongo jana (Jumatano) ni mpango wa serikali wa kuwafurusha maskwota kutoka ardhi ya East Africa Portland. Mwaweza kuteketeza kila kitu lakini mjue kwamba tutawaondoa. Nitaelekea huko leo (jana Alhamisi),” akasema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

CHARLES WASONGA, KEVIN CHERUIYOT na MWANGI NDIRANGU

  • Tags

You can share this post!

Zetech Sparks yalenga kusuka kikosi ipate kani kali za...

KASHESHE: Femi One kampata mtu wake

T L