• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:42 PM
Shahbal avunja nyoyo za wafuasi kwa kujiondoa uchaguzini

Shahbal avunja nyoyo za wafuasi kwa kujiondoa uchaguzini

NA WINNIE ATIENO

SIKU chache baada ya kujiuzulu kugombania ugavana wa Mombasa, Suleiman Shahbal aliyeashiria angesimama kama mgombeaji huru, amebadilisha nia na kutangaza kuwa atamuunga mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir.

Awali, Bw Shahbal ambaye alishurutishwa kuwania kiti hicho kama mgombea huru, aliwahakikishia wafuasi wake sugu kwamba angekaa chini na kamati yake kutafuta mwelekeo.

Lakini kwenye hafla ya kula futari ya Gavana Hassan Joho ambapo kinara wa ODM Bw Odinga alialikwa, Bw Shahbal alizima matumaini ya wafuasi na mgombea mwenza wake kurejea kwenye kinyang’anyiro hicho.

Bw Shahbal alipigia debe chama cha ODM akiwarai wakazi kukiunga mkono.

“Ninawasihi kusimama na chama cha ODM na kuhakikisha Mombasa ambacho ni kitovu cha chama hiki kinasalia,” alisema.

Bw Shahbal aliahidiwa nafasi nzuri ya kazi katika serikali ya Bw Odinga.

Baada ya Bw Shahbal kukubali kumpigia debe Bw Nassir, wafuasi wake, wakiongozwa na mgombea mwenza, Bi Selina Maitha walimwambia asikubali kumwachia Bw Nassir na badala yake waendelee na siasa zao kama wagombea huru.

Bi Maitha aliongea kwa huzuni akisema wafuasi wa Bw Shahbal wamekasirika kwa hatua aliyoichukua.

“Watu wanahisi uchungu sababu wanakuona kama wewe ndio mkombozi. Msheshimiwa tunakuhitaji, badilisha nia twende kama wagombea huru,” alisema Bi Maitha ambapo wafuasi wake walianza kusheherekea.

Bi Maitha ambaye alikuwa naibu kamishna wa kaunti alijiuzulu wadhifa wake kugombea siasa za Mombasa.

Wafuasi sugu wa Bw Shahbal walimlilia kutokubali uamuzi wa chama cha ODM.

“Kwanini Bw Odinga anakuambia ujiuzulu? Wewe ni wa wananchi sio wa Baba, tumekuwa watumishi miaka mingapi katika hii kaunti. Lazima usimame kama mwanamume, tumechoka kuwanyenyekea watu kadhaa hapa Mombasa, kaunti haina maendeleo. Hakuna kitu kitabadilika,” alisema mwanasiasa Amina Mohammed.

Bi Mohammed ambaye anagombea kiti cha uwakilishi wa wanawake kupitia chama cha Jubilee alisema alisikitishwa na hatua ya Bw Shahbal.

Bw Shahbal alishindwa kujieleza baada ya kuona wafuasi wake wakimlilia.

“Nimekutana na wafuasi wangu na nikawaeleza sababu zangu kujiuzulu kwenye kinyanganyiro hiki cha ugavana. Kwa mara nyingine tena nataka kuwashukuru kwa kusimama na mimi tangu nilipoanza hatua hii miaka 12 iliyopita,” alisema Bw Shahbal.

Hata hivyo aliwahakikishia wafuasi wake kwamba atakaa na kamati yake kuamua mwelekeo wake.

Usemi huo ulizua bashasha kwenye ukumbi wa Tononoka ambako alitangaza hatua yake.

“Ulipokuwa ukitafuta ugavana ulitutafuta tukufanyie kampeni, mbona hukutueleza? Ungetuitia huyo Bw Odinga kwanza tukae naye, sivyo uamuzi wako hauwezekani,” alisema Bi Margaret Ambasa mfuasi wake sugu.

Wengine walisema waliumwa na hatua hiyo baada ya kujitolea mhanga kumfanyia kampeni na baadaye akajiondoa kwenye kinyanganyiro hicho.

Wiki iliyopita Rais Kenyatta na kinara wa ODM walimwidhinisha Mbunge wa Mvita kugombea ugavana wa Mombasa.

  • Tags

You can share this post!

Ukoo wa Jaramogi wavuna tiketi za ODM kuwania vyeo Agosti

Helikopta yaibua msisimko katika kampeni za Muthama

T L