• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Shinikizo zazidi kwa Kalonzo ajiunge na Ruto

Shinikizo zazidi kwa Kalonzo ajiunge na Ruto

NA PIUS MAUNDU

SHINIKIZO zinaendelea kutolewa kwa Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ahame muungano wa Azimio la Umoja na ajiunge na mrengo wa Kenya Kwanza, unaoongozwa na Rais Mteule, Dkt William Ruto.

Wakazi na baadhi ya wabunge kutoka Ukambani ndani ya Wiper wanamtaka Bw Musyoka aungane na Dkt Ruto kwa sababu wanaona itakuwa vigumu kumshinda kwenye kura za 2027 na 2032.

Katika mkutano wake wa mwisho Ukambani ambalo ni eneo Bw Musyoka anajivunia ufuasi mkubwa, Dkt Ruto aliahidi kumhusisha Bw Musyoka katika uongozi wake iwapo angeshinda Urais.

“Pamoja na Gavana wa Machakos Alfred Mutua, tumeamua kumshirikisha Bw Musyoka katika serikali yetu,” alisema Dkt Ruto katika kituo cha kibiashara cha Kalamba, Kaunti ya Makueni.

Wakati huo katika misururu ya mikutano aliyohutubia Ukambani, Dkt Ruto alisisitiza kuwa, Bw Musyoka anastahili kuhama mrengo wa Azimio la Umoja kwa sababu Bw Odinga alikuwa na nia ya kuzima ndoto yake kisiasa.

Bw Musyoka naye alimjibu Dkt Ruto kwa kudai alikuwa anatumia jina lake kujipendekeza kwa wapigakura wa eneo hilo ili avutie uungwaji mkono.

Kufuatia ushindi wa Dkt Ruto, wakazi na baadhi ya viongozi wamemtaka Bw Musyoka atalikiane na Bw Odinga na kujiunga na utawala wa Dkt Ruto.

“Bw Musyoka anastahili kujiunga na kambi ya Kenya Kwanza ili eneo letu lisitengwe kimaendeleo,” akasema Bw Ambrose Mbiti kutoka Mwingi, Kaunti ya Kitui.

“Kama Wakamba, hatutakubali kukaa nje ya serikali. Kama viongozi tushauriane na Rais Mteule ili kuwe na mkataba mzuri na hii itawezekana iwapo Bw Musyoka ataungana na mrengo wa Dkt Ruto,” akasema mwaniaji kiti cha eneobunge la Kaiti kupitia ODM Sila Kaloki.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa Wiper wamepinga madai kuwa Bw Musyoka yupo njiani kujiunga na Kenya Kwanza, wakitaja habari hizo kuwa propaganda.

“Hiyo ni propanganda na haiaminiki,” akasema mbunge mmoja wa Wiper ambaye hakutaka jina lake linukuliwe kwa sababu haruhusiwi kuzungumza kwa niaba ya chama hicho.

Madai kuwa Dkt Ruto anamvizia Bw Musyoka yalianza kushika kasi wiki hii baada ya baadhi ya wabunge kutoka ngome yake ya Ukambani ambao walichaguliwa kwa tikiti ya Maendeleo Chap Chap yake Dkt Mutua kuhamia Kenya Kwanza.

Ikizingatiwa ana magavana watatu, maseneta watatu na wabunge 22, wadadisi wa kisiasa wanahoji kuwa Bw Musyoka atakuwa amemsaidia Dkt Ruto kupata uungwaji mkono wa kutosha bungeni ili apitishe ajenda zake za kisiasa.

“Maendeleo Chap Chap imeamua kujiunga na Rais mteule Dkt William Ruto katika muungano wa Kenya Kwanza. Hatutaki watu wetu wawe upinzani kwa sababu tuna hakika ushindi wa Dkt Ruto hautabatilishwa,” akasema mbunge mteule wa Kibwezi Mwengi Mutuse.

Alikuwa ameandamana na mbunge wa Machakos Mjini, Caleb Mutiso.

Kando na wabunge hao, wenzao saba pamoja na wengine 10 waliochaguliwa bila vyama wameonyesha uaminifu wao kwa Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Tumepata ushahidi wa kubatilisha ushindi wa Ruto –...

Mashirika ya kijamii yasema uchaguzi wa Agosti 9 ulisheheni...

T L