• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Shirika lataka wagombea urais watie saini mkataba wa kudumisha amani

Shirika lataka wagombea urais watie saini mkataba wa kudumisha amani

NA BENSON MATHEKA

KUNDI moja la kijamii nchini limewataka wagombeaji wa urais kuahidi kwamba wataendesha kampeni za amani, kukubali matokeo ya uchaguzi na kudumisha amani baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Kuungana, Kujenga Kusaidia Kenya (KKKK) linasema kwamba Wakenya hawataki kushuhudia ghasia baada ya uchaguzi mkuu mbali wanataka amani ili kuendelea na shughuli za kujenga uchumi.

“Sisi kama shirika la kijamii tunataka wagombeaji wa urais wote wane na manaibu wao, kuapa kwa kutia saini mkataba na Wakenya kwamba watadumisha amani kwa kuhakikisha wafuasi wao watadumisha utulivu katika kampeni zao, kwenye uchaguzi na baada ya uchaguzi mkuu,” asema Katibu Mkuu wa shirika hilo David Kimengere Waititu.

Anasema kwamba atapeleka mkataba huo kwa wanasiasa hao wote ambao wanapaswa kutia saini kuapa hawatachochea na kufadhili vijana kuzua ghasia.

“Kenya nchi yetu ni kubwa kuliko mwanasiasa na mrengo wa kisiasa. Ni lazima tuilinde kwa hali na mali. Katika Kuungana, Kujenga na Kusaidia Kenya tunachukulia hili kuwa jukumu letu,” akasema.

Wagombeaji wa urais katika uchaguzi wa mwaka huu ni Raila Odinga wa Muuungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Naibu Rais William Ruto wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Prof George Wajackoyah wa chama cha Roots Party na Mwaure Wahiga wa chama cha Agano.

Bw Kimengere anasema shirika lake linataka wadau katika uchaguzi mkuu kupiga marufuku wagombeaji urais ambao watachochea ghasia nchini.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Wanakuza miche inayovutia hata wateja nchi za nje

UJASIRIAMALI: Watengeneza miswaki kwa mianzi kulinda...

T L