• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
ZARAA: Wanakuza miche inayovutia hata wateja nchi za nje

ZARAA: Wanakuza miche inayovutia hata wateja nchi za nje

NA LABAAN SHABAAN

ALIPONUNUA shamba takriban miaka 20 iliyopita, Lister Kinuthia hakudhania shamba hilo lingemzalishia matunda tele na ufanisi maishani mwake.

Ungemueleza kuwa shamba hilo la robo tatu ya ekari alilonunua Kiserian Kajiado lingesheheni bustani kubwa ya miche ainati inayovutia wateja nje ya wigo wa Kenya, asingeamini.

Kwa kukumbatia mifumo dijitali ya mauzo ya mazao, Mkurugenzi wa Gad Eden Seedlings and Nurseries, Lister Kinuthia, ametanua mbawa za kampuni hii kunasa wateja mbali na Kaunti ya Kajiado.

Masoko yao ima ya kusambazia miche ama ya kufunza mitindo ya ukuzaji yamo Kenya, Uganda, Rwanda, Ghana, Tanzania na Nigeria.

Mitandao ya kijamii hasa kupitia kampuni ya ufikiaji masoko kidijitali ya Mkulima Young, iliwasaidia sana katika maenezi ya kazi wanayofanya tangu walipoanza.

Maryanne Kinuthia, Afisa wa Masoko, ni binti yake Mkurugenzi wa kampuni hii. Jinsi anavyofurahia kilimo ni kielelezo bora kwa vijana walioambaa shughuli za zaraa.

“Tulianza kwa changamoto nyingi. Hatukujua njia mwafaka za kukuza miche. Tukipanda ilikuwa inaharibika ikabidi tukafanya utafiti kisha tukafaulu,” anasema Maryanne.

“Safari yetu yenye pandashuka ilitufanya tukaamua kufunza wakulima wengine kuhusu utunzaji wa miche ili wasipate shida sawa na zetu tulipolianza kilimo,” anasema.

Miongoni mwa miche inayokuzwa hapa ni ya sukuma, kabeji, pilipili mboga, nyanya, miti ya matunda kama vile miparachichi na michungwa, viungo kama vile basil na kadhalika.

Miche inayoandaliwa hapa huchukua kati ya wiki tatu na nne kukua na kuwa tayari kwa upandikizaji. Mingine inapandikizwa Gad Eden huku mingi ikiuzwa kwa wateja. Ufanisi wa ukuaji wa miche kwa trei maalum ni asilimia 98, wanaeleza wakulima hawa.

Shambani humu kuna maelfu ya vitalu vya miche. Kila trei ina mimea mia mbili na mche mmoja huwa na bei kati ya Sh2- Sh10 kwa kuwa hutegemea aina ya mmea.

“Siwezi kuwaambia inatugharimu pesa ngapi kuendeleza shughuli humu lakini ni muhimu mfahamu kuwa mimea hii inaleta pesa haraka kwa sababu inakua baada ya muda mfupi,” Maryanne anaambia Akilimali.

Mtaalamu wa miche na mkulima katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo na Teknolojia JKUAT, John Karika anasema trei moja ya miche ya sukuma wiki yenye seli 128 huzalisha faida ya kati ya Sh150 na Sh200 kila mwezi hivyo ukiwa na trei 100 utapata hadi Sh20,000.

“Soko la miche Kenya ni kubwa sana. Kile kinachohitajika kwa mkulima ni kuongeza viwango na kukuza kwa mfululizo,” Karika anaeleza.

Aghalabu wateja wa Kinuthia huenda shambani humo kununua bidhaa kila siku na endapo watahitaji kuuziwa wakiwa mbali, kampuni hii huwasafirishia hadi waliko.

Gad Eden inalea sehemu ya mimea hii ndani ya vivungulio na mingine kwenye shamba wazi.

“Ni nadra sana kwa mteja kufika huku na kukosa miche. Mimea iko katika hatua tofauti za makuzi na kwa hivyo kila siku ni siku ya mauzo,” anaeleza mkurugenzi wake.

Kwa mujibu wa Synnefa, kampuni ya kusuluhisha matatizo ya wakulima kiteknolojia, kivungulio cha mita 40 mraba kilichoundwa kwa mbao hugharimu Sh72,000.

Kwa msimu wa miezi 9 kinaweza kuzoa mapato ya hadi Sh240,000.

Kadhalika Synnefa hukitia wakulima kivungulio cha vyuma kwa Sh112,000 na huzalisha mapato sawia.

“Sasa tuna mbinu dijitali ya kuwezesha mkulima kuchagua kivungulio mwafaka kulingana na uwezo wake na kiasi cha shamba na ukubwa wa kivungulio,” Afisa Mkuu wa Synnefa, Taita Ngetich anaarifu.

Lister anatueleza kuwa Gad Eden huandaa warsha kufunza wakulima wengine jinsi ya kukita vijishamba na vitalu kwa sababu soko ni kubwa na bado halijatoshelezwa.

Wafanyakazi wa Gad Eden wakiandaa vitalu. PICHA | LABAAN SHABAAN

Siku za usoni shamba hili linalenga kuongeza ukubwa wa ardhi na kuzalisha miche mingi ili kutosheleza soko linalokua Kenya na nje ya nchi.

“Huwa tunawapa wanafunzi wetu wa kilimo wateja wakati wanaanza ili wakue kwa sababu shamba letu lina wateja sehemu nyingi ya Kenya na nje ya nchi,” Lister anasema.

“Tunalenga kuzidisha uzalishaji siku zijazo kwa sababu utashi wa malisho mabichi na yenye afya unapanda,” anaongeza.

Shamba hili la Kajiado hukuza mimea kwa mitindo mseto; wenyeji hukumbatia matumizi ya mifumo asili ya upanzi na pia matumizi ya kemikali ya kisasa. Yote haya yanakwenda kulingana na matakwa ya wateja wao.

  • Tags

You can share this post!

Raila ashawishi Ngilu kujiondoa kura ya ugavana

Shirika lataka wagombea urais watie saini mkataba wa...

T L