• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:55 AM
UJASIRIAMALI: Watengeneza miswaki kwa mianzi kulinda mazingira

UJASIRIAMALI: Watengeneza miswaki kwa mianzi kulinda mazingira

NA MARGARET MAINA

WANANDOA Atiff Ibrahim Khalid na mkewe Natasha Lakhani, wamejiingiza katika soko linalozingatia mazingira, na kutengeneza miswaki ya mianzi (bamboo) na dawa za meno za kikaboni.

Wanandoa hao waliingilia ujasiriamali huu baada kuzuru Thailand mnamo 2019.

“Tulistaajabishwa na jinsi katika ulimwengu unaotatizwa na plastiki, watu wa Thailand walikuwa wakitumia mianzi katika bidhaa za kila siku ili kufanya nafasi yao ndogo duniani kuwa bora,” anasema Khalid.

Walijua walipaswa kutumia maarifa yao mapya ili kuboresha mazingira yao na baada ya kufanya utafiti, mwaka wa 2020 walianzisha kampuni ya Ecosmiles Limited, kampuni inayotengeneza miswaki kwa kutumia mianzi na DuPont bristles, ambayo imetengenezwa kwa nailoni lakini ina muda maalum wa kutumika.

Kampuni hiyo inatengeneza bidhaa za utunzaji kinywa kwa njia ya kibinafsi ambazo ni mbadala kwa zile za plastiki zinazopatikana sokoni, nyingi zikiwa huishia baharini kama takataka. Walianzisha biashara yao kwa mtaji wa Sh5.5 milioni.

Kampuni hiyo ina kituo cha uzalishaji na uundaji bidhaa Vipingo, Kilifi na ofisi yake kuu katika mtaa wa Parklands, Nairobi.

“Tangu wakati huo tumewekeza zaidi ya Sh8 milioni kwenye biashara yetu huku tukiendelea kutafuta fedha kutoka kwa wawekezaji wetu tuliowapata hivi karibuni ambao wamekuwa na jukumu kubwa katika kutoa ushauri na kuelekeza fedha katika ukuaji na upanuzi wetu.”

Miswaki inatengenezwa kutoka kwa mashina ya mianzi kwa mashine maalumu, kulingana na ukubwa tofauti.

Miswaki kutokana na mianzi. PICHA | MARGARET MAINA

Wanapata mianzi kutoka kwa wakulima wanaokuza mianzi kibiashara huko Kilifi.

“Kila mianzi iliyokatwa hupandwa tena na nyenzo za ziada hutumiwa kupasha joto kiwanda.

“Miswaki hiyo ina nailoni laini ambayo ni nzuri katika kusafisha meno bila kuharibu ufizi.”

Miswaki, kwa ajili ya usafi mzuri wa kinywa inashauriwa kubadilishwa kila baada ya miezi mitatu na ni bora kubuni upya miswaki iliyochakaa.”

Wameongeza uwezo wa uzalishaji katika kituo chao kutoka miswaki 1,000 walipoanza, hadi vipande 10,000 kwa mwezi ili kutimiza maagizo huku habari zikienea kuhusu bidhaa zao katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Bei ya bidhaa zao ni kati ya Sh170 hadi Sh900. Miswaki yao ya mianzi inauzwa Sh299 kwa watu wazima na Sh249 kwa watoto.

Pia hutoa bei ya jumla kwa wanunuzi wa jumla na wachuuzi wadogo. Anaongeza kuwa ubinafsishaji unaweza kufanywa kwa hoteli na kampuni nyingine.

Kando na miswaki, wao pia hutengeneza dawa za meno, ambazo huzihifadhi katika vidude viliyoundwa kwa glasi vinavyoweza kutumika zaidi ya mara moja. Wateja wanaojisajili nao pia huweza kujaziwa tena dawa hiyo ya kusafisha meno.

Khalid anasema wanapata dawa za meno kutoka Thailand lakini wanatarajia kuanza uzalishaji nchini mara tu watakapopata mashine zinazofaa.

“Vidonge vyetu vyote vya dawa ya meno vimetengenezwa kwa viambato vya kikaboni kama vile mafuta ya nazi. Mtoto hatakua na shida akimeza.Hazina vihifadhi wala nyongeza,” Khalid anasema.

Pia wanatengeneza brashi ya nywele, bidhaa za kusafisha meno kutokana na mkaa na unga wa nazi.

Gramu 30 huuzwa kwa Sh399.

“Tumekuwa na mauzo mazuri tukiwa na viwango vya faida lakini kwa sasa, tumejipanga zaidi katika ukuaji wa biashara na upanuzi badala ya kupata faida pekee.”

Eco-Smiles ina wafanyakazi saba wa kudumu ambao huchukua majukumu makuu ya kampuni na wanaajiri kati ya wafanyakazi 20 hadi 30 wa vibarua.

Hata hivyo, anaeleza kuwa hawajakosa changamoto wakijaribu kupenyeza katika soko hilo.

Khalid aliteuliwa kama mshindi wa fainali ya tuzo za mwanzilishi wa mwaka wa 2021 kati ya nchi 7 za Afrika (FOYA), na aliwakilisha Kenya katika UNEP Dubai 2021.

  • Tags

You can share this post!

Shirika lataka wagombea urais watie saini mkataba wa...

Wawaniaji wa urais washawishi majopo ya IEBC yawarudishe...

T L