• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Sonko alilia jopo limruhusu awanie ugavana Mombasa

Sonko alilia jopo limruhusu awanie ugavana Mombasa

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA gavana wa Nairobi Mike Sonko mnamo Jumatano aliambia jopo la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) la kuamua mizozo ya uteuzi wa wawaniaji wa nyadhifa za uongozi (DRC) liamuru akubaliwe kuwania ugavana Mombasa kwa vile hakuna agizo la mahakama linalomzuia.

Mawakili Dkt John Khaminwa, Wilfred Nyamu na Assa Nyakundi pamoja na mawakili wa chama cha Wiper Eunice Lumallas, Kevin Katisya na Arnold Oginga walisema “hakuna agizo kutoka kwa mahakama yoyote linalomzuia Sonko kuwania ugavana Mombasa.”

Lumallas alisema matamshi ya mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kwamba Sonko alitimuliwa mamlakani kwa sababu ya ufisadi na bunge la Seneti ndiyo yalifanya afisa msimamizi wa uchaguzi wa Mombasa (CRO) Bi Swalha Ibrahim Yusufu kutomwidhinisha (Sonko).

Lakini IEBC na Tume ya Kukabili ufisadi nchini (EACC) ziliunga mkono uamuzi wa CRO zikisema,“Sonko hastahili kuidhinishwa kwa vile alitimuliwa uongozini kwa sababu ya ufisadi.”

Pia Swalha alisema Sonko hakuwasilisha cheti asili cha digrii kutoka chuo kikuu cha KeMU.

Hata hivyo, Sonko alishikilia kuwa ameonewa na haki za watu wa Mombasa kumchagua kiongozi wanayempenda zimekiukwa na uamuzi wa CRO.

Sonko alisema amekandamizwa na jopo hilo linapasa kuzingatia kuwa amekata rufaa katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi wa bunge la Seneti kumtimua mamlakani kwa sababu ya ufisadi na matumizi mabaya ya afisi yake.

Huku Sonko akiendelea kupambana kujinusuru, wawaniaji wa ugavana Nairobi (Polycarp Igathe) na Murang’a (Dkt Irungu Kang’ata) walikubaliwa kuwania baada ya malalamishi dhidi yao kufutiliwa mbali.

Seneta Irungu Kangata afurahia ushindi katika kesi ya kupinga yeye kuwania ugavana Murang’a. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Naye mwaniaji wa chama cha UDA, ugavana Nairobi Johnson Sakaja hajui hatima yake kwa vile Tume ya kusimamia Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) imekataa kutambua cheti cha digirii cha chuo kikuu cha Team University cha Uganda.

Kitumbua cha Sakaja kimetiwa mchanga zaidi na ushahidi kutoka Chuo kikuu cha Nairobi (UoN) kwamba hakukamilisha masomo chuoni humo.

Jopo linalosikiliza kesi ya Sakaja likiongozwa na Bw George Mburugu limepokea mawasilisho kwamba amehitimu na walalamishi katika kesi hiyo wanatumiwa kumvuruga kisiasa.

Sakaja anayewakilishwa na Elias Mutuma ameomba jopo hilo litupilie mbali malalamishi hayo kwa vile seneta huyu amehitimu kwa shahada ya digrii na hata chuo cha Teams University cha Uganda kilithibitisha kwamba alisoma huko.

Bw Igathe alikubaliwa kuendelea na azma yake baada ya kutupiliwa mbali kwa kesi iliyopinga uteuzi wake na chama cha Jubilee kuwania ugavana Nairobi.

“Hili jopo haliwezi kusitisha uteuzi wa Igathe kutokana na madai kuwa alijiuzulu wadhifa wa naibu wa gavana wakati wa enzi ya Sonko,” lilisema jopo lililoongozwa na Wambua Kilonzo, Irene Masitsi na Justus Nyang’aya.

Jopo hilo pia lilisema kwamba uteuzi wa Dkt Kang’ata kuwania ugavana Murang’a pamoja na naibu wake Stephen Mburu haukukinzana na sheria. Igathe na Kang’ata sasa wanatarajiwa kutifua kivumbi cha kampeni.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali iwakabili wanaoharibu sifa ya vyeti vya...

Wanawake wanadandia wanasiasa ‘kupata riziki’

T L