• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Wanawake wanadandia wanasiasa ‘kupata riziki’

Wanawake wanadandia wanasiasa ‘kupata riziki’

NA FARHIYA HUSSEIN

WANAWAKE eneo la Pwani wametaja hali ngumu ya maisha kuwa sababu kuu ya wao kuhudhuria mikutano ya hadhara ya kisiasa ambayo kwa muda mrefu imehusishwa na vijana na wanaume.

Bi Amina Abdallah kutoka Kaunti ya Mombasa alieleza kuwa, huwa wanalazimika kuacha kazi zao za nyumbani ili wahudhurie mikutano ya kisiasa ndipo angalau wapate fedha za kujikimu nyakati hizi ngumu.

“Kinachonifanya nihudhurie mikutano ya hadhara si mapenzi yangu kwa wanasiasa, bali ni pesa ninazopata kutoka humo. Kwa nini nibaki nyumbani wakati naweza kupata Sh500 mwisho wa siku hiyo kwa kujitokeza tu kwenye mikutano ya kampeni?” akauliza Bi Abdallah.

Wao huanza kujiandaa kwa kukutana kwa makundi kukubaliana kuhusu maandalizi ikiwemo mavazi watakayovaa.

Mwaka huu 2022, imebainika makundi mengi ya wanawake hupendelea kuvaa dera zilizo na rangi ya chama au muungano wa kisiasa wanaohudhuria mkutano wake.

“Baada ya mgombea wa kisiasa kutangaza kuwa atakuwa na mkutano siku fulani, tunakutana na kujadili kanuni za mavazi. Kawaida ni dera lakini rangi lazima ilingane na chama cha siasa ambacho tutaunga mkono siku hiyo,” akasema Bi Abdallah.

Kauli sawa na hii ilitolewa na Bi Nyabwana Ahmed, kutoka Kaunti ya Lamu ambapo mbinu kuu inayotumiwa na wanawake ni utungaji wa nyimbo na mashairi ili kuwasifu au kuwakosoa wanasiasa.

“Si lazima mtu kuwa mwanamuziki kufanya hivyo. Wakati mwingine tunaunda kwa nyimbo za kitamaduni kwa sababu zina ujumbe na maana zaidi,” alisema Bi Nyabwana Ahmed.

Wanawake hao walieleza kuwa, ni lazima wafanye kazi zaidi ili kupokea malipo mwisho wa siku.

“Bei za bidhaa nyingi zimepanda. Kwa mama ambaye ni mlezi wa kipekeee na hana usaidizi hana budi ila kuhudhuria mkutano hii kupata riziki,” alisema Bi Ahmed.

Katika Kaunti ya Kilifi, vikundi vya wanawake havijaachwa nyuma.

Tofauti na Mombasa, wanawake hapa wanapendelea kuvalia leso ambazo zina rangi husika ya kisiasa.

Leso hizo huwa na maandishi ya methali na mafumbo ya Kiswahili ambayo yanahusiana na ujumbe wa kisiasa unaotolewa kwenye mikutano ya hadhara.

Baadhi ya zile maarufu zaidi ni “Usimuone simba amenyeshewa ukadhani ni paka”, na “Mlala hoi hana haki”.

Kulingana na Bi Beatrice Kazungu ambaye ni mmoja wa viongozi wa hivi vikundi vya wanawake majadiliano huhusisha idadi ya wanawake wanaohitajika katika mkutano wa kisiasa na kiasi cha pesa ambacho kila mmoja atalipwa.

“Kupitia kwa kiongozi wao, wanawake basi hukutana na kujadili rangi ya mavazi watakayovaa siku hiyo. Lakini inafaa liwe vazi la dera au leso. Kwa sababu fulana zinatumika sana na wanaume,” asema Bi Kazungu.

Kulingana na Mtendaji Mkuu wa Mtandao wa Wanawake wa Mashinani, Bi Carol Oduor, ndoa nyingi zimekuwa hatarini kwa sababu ya wanawake kupuuza majukumu yao ya nyumbani ili kuhudhuria mikutano ya kisiasa.

“Kipindi hiki cha uchaguzi tumepokea kisa ambapo mwanamke amerudishwa kwao nyumbani mara mbili kwa sababu ya kuzembea nyumbani na majukumu yake kama mke,” akasema Bi Oduor.

Wanawake hao wanasemekana kuondoka nyumbani mapema ya saa kumi na mbili asubuhi na kurejea majira ya saa nne usiku.Anabainisha wakati wa uteuzi, walirekodi visa vitatu vya wazazi kutengana katika eneo bunge la Changamwe kutokana na wake zao kujihusisha na mikutano za siasa.

Mikutano kadha maeneo mbalimbali ya Pwani kufikia sasa imeshuhudia fujo ambapo majeraha yalisababishwa na mkanyagano wa watu, huku mkutano mmoja wa hapo awali ukisababisha kifo cha mtu mmoja.

Katika mkutano wa kuadhimisha siku ya wanawake ulimwenguni ambao uligeuzwa kuwa wa kisiasa Mombasa, makundi ya wanawake yalivamiana kila upande ukitetea mwanasiasa tofauti.

  • Tags

You can share this post!

Sonko alilia jopo limruhusu awanie ugavana Mombasa

DARUBINI YA UKWELI: IEBC ndiyo hudhibiti Sajili ya...

T L