• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
TAHARIRI: Serikali iwakabili wanaoharibu sifa ya vyeti vya masomo ya vyuo

TAHARIRI: Serikali iwakabili wanaoharibu sifa ya vyeti vya masomo ya vyuo

NA MHARIRI

UJASIRI wa mwaniaji urais wa chama cha Safina, Jimi Wanjigi kufichua udhaifu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), umefungua ukurasa mpya wa jinsi mambo yanastahili kufanywa hapa Kenya.

Bw Wanjigi mnamo Jumatatu Juni 6, alitoa taarifa iliyoonyesha wazi kuwa, labda kulikuwa na uzembe au ufisadi ndani ya IEBC. Maafisa wa tume hiyo walikuwa wamempitisha Bw Walter Mong’are wa chama cha Umoja Summit.

Iligundulika baadaye kuwa Bw Mong’are alikuwa amekubaliwa kuwania urais ingawa hakuwa amekamilisha masomo ya digrii. Alikuwa angali mwanafunzi sawa na Bw Wanjigi.

Tangu wakati huo, IEBC imefuatilia kwa makini na kutambua kwamba hata anayetamani ugavana Nairobi kwa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Bw Jonson Sakaja, hakukamilisha masomo ya digrii katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Tume ya Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) imesema haitambui cheti cha digrii kutoka Chuo Kikuu cha Team nchini Uganda, ambacho Bw Sakaja alitaka kutumia kuwania ugavana.

Si yeye pekee, kuna wanasiasa wengi ambao huenda kwa kutotaka ugavana au urais, tunawachukulia kuwa vyeti vyao vya digrii ni halali.

Ufichuzi huu unatia wasiwasi Wakenya masikini wanaong’ang’ana katika vyuo vikuu vyetu na baadaye kuishia kumaliza visigino wakitafuta ajira. Wasiwasi huo unatokana na kuwa, watu walio na pesa huenda walitumia ushawishi wao kupata au kununulia watoto wao vyeti katika taaluma zinazohusiana na maisha ya wananchi.

Kama kwa mfano mtu alinunua cheti kuonyesha ni daktari wa upasuaji ilhali alikuwa akitoroka darasani wakati wa masomo chuoni, kuna uhakika gani kuwa akifanyia mgonjwa oparesheni itamalizika salama?

Barabarani, madereva waliojifunza magari vichochoroni na baadaye wakaenda kufanya mtihani au kununua leseni za udereva, ni hatari kwa maisha ya abiria.

Mifano ni mingi ya hasara iyoweza kusababishwa na waliopata vyeti kwa njia ya mkato.

Kinachohitajika sasa, ni kwanza serikali iwachukulie hatua wote waliodanganya kuhusu vyeti vyao. Pili, iwapo kuna taasisi iliyohusika na udanganyifu huo, maafisa husika pia wakabiliwe na mkono wa sheria.

CUE inapaswa kuchunguza maafisa wake na kuhakikisha kuwa, hakuna anayeidhinisha kozi au cheti bila ya kufuata misingi iliyowekwa.

Iwapo serikali haitaonyesha ubaya wa matendo ya wanasiasa wanaokabiliwa na tuhuma, itakuwa imeweka msingi hatari kwa watoto wetu.

Mwishowe, hakuna mtu atakayethamini kutoa bidii masomoni. Kila mtu atakuwa akitafuta njia za mkato za kupata vyeti, ambavyo mwishowe vitakuwa mwanzo wa maangamizi kwetu kama taifa.

  • Tags

You can share this post!

Wito wafungwa washauriwe kabla kuachiliwa

Sonko alilia jopo limruhusu awanie ugavana Mombasa

T L