• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Sonko azidi kusukuma IEBC muda ukiyoyoma

Sonko azidi kusukuma IEBC muda ukiyoyoma

ANTHONY KITIMO NA VALENTINE OBARA

HATIMA ya kisiasa ya gavana wa zamani wa Nairobi, Bw Mike Sonko, kuwania ugavana Mombasa, ingali gizani huku muda ukizidi kuyoyoma kuelekea uchaguzi wa Agosti.

Bw Sonko alirejea kwa maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Mombasa, Jumatano baada ya kukosa kuidhinishwa kuwania kiti hicho Jumanne.

Duru ziliambia Taifa Leo kuwa, mawakili wa Bw Sonko wanaendelea kutumia muda wao mwingi ili kunusuru nyota yake ya kisiasa inayoelekea kuzimwa.

Ijapokuwa alitarajiwa kufika mbele ya IEBC Jumatano asubuhi, alienda huko mwendo wa saa kumi na moja jioni.

Aliwasilisha vyeti vya kuthibitisha kuwa, ana rufaa aliyokata katika Mahakama ya Juu dhidi ya uamuzi wa Bunge la Kaunti ya Nairobi kumtimua mamlakani mwaka wa 2020.

Kulikuwa na sarakasi tele Jumanne wakati mwanasiasa huyo alikataa kuondoka katika kituo cha IEBC kilicho katika mtaa wa Kizingo, akisisitiza lazima apewe cheti cha uwaniaji.

Baadaye usiku, maafisa wa IEBC walimshawishi kuondoka na kumwomba arudi Jumatano (jana) ili washauriane zaidi kuhusu hatua ambazo angetakikana kuchukua.

Bw Sonko alikuwa akijitetea kwamba, rufaa yake katika Mahakama ya Juu inamaanisha kuwa, hafai kuchukuliwa kama mtu aliye na hatia hadi uamuzi utakapotolewa katika kesi hiyo.

“Sheria inafaa itekelezwe kwa usawa kwa Wakenya wote. Haifai iwe eti kuna sheria inayomsimamia Sonko na sheria nyingine inayosimamia wanasiasa wengine,” akasema, akidai kuwa wanasiasa wengine walipatwa na hatia mahakamani wamekubaliwa kuwania kwa vile wamekata rufaa dhidi ya hukumu zao.

Mahakama ya Juu inatarajiwa kutaja rufaa yake kesho Ijumaa.

Msimamizi mkuu wa uchaguzi Mombasa, Bi Swalhah Yusuf, alikuwa amesema hakuwa amepokea agizo lolote la mahakama kutaka IEBC imwidhinishe Bw Sonko, kinyume na vile mawakili wake walikuwa wakidai.

Bi Yusuf alitaka Bw Sonko na mawakili wake waelekee kwa kamati ya kutatua mizozo kati ya wanasiasa na IEBC, ambayo itaanza vikao vyake kesho.

“Maagizo ambayo tunayo kutoka kwa Mahakama Kuu ni yale ambayo yalizuia IEBC kumwidhinisha Bw Sonko kwa sababu za Kikatiba. Tukipata maagizo mapya, tutayafuata,” akaeleza Bi Yusuf.

Kufikia Jumanne ambapo IEBC ilifunga shughuli ya kuidhinisha wawaniaji ugavana, wanasiasa saba walikuwa wamehitimishwa kushindania kiti cha Gavana Hassan Joho.

Saba hao ni Bw Daniel Kitsao (mwaniaji huru), aliyekuwa seneta, Bw Hassan Omar (UDA), Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi (PAA), aliyekuwa mbunge wa Nyali, Bw Hezron Awiti (VDP), Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir (ODM) na Bw Shafii Makazi (mwaniaji huru).

Kura za maoni zimekuwa zikionyesha kuwa, ushindani wa karibu ungetarajiwa kati ya Bw Nassir na Bw Sonko katika kinyang’anyiro hicho.

  • Tags

You can share this post!

Ruto amponda Raila kuhusu mitumba

Polisi walioua 4 Masimba watiwe mbaroni, viongozi washikilia

T L