• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Suala la sava za IEBC lisifike meza ya mazungumzo, Gachagua aonya Azimio

Suala la sava za IEBC lisifike meza ya mazungumzo, Gachagua aonya Azimio

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa anaonekana kubadili msimamo wa kupinga mazungumzo ya maridhiano kati ya mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio, ila anatoa mapendekezo kuhusu ajenda za kujadiliwa.

Akiongea katika eneo la Laare, kaunti ya Meru wakati wa ibada ya Jumapili Bw Gachagua alisema kuwa ajenda ya utathmini wa matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2022 haifai kujadiliwa.

Kulingana na Naibu Rais, matokeo hayo tayari yalikwisha kutathminiwa na Mahakama ya Upeo iliyobaini kuwa Rais William Ruto alishinda uchaguzi wa urais kwa njia halali.

“Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo inayoketi kule Bomas inafaa kuondoa suala hili kutoka kwa ajenda ambazo itashughulikia. Sababu ni kwamba suala hilo liliamuliwa kisheria na Mahakama ya Upeo na halifai kujadiliwa tena,” Bw Gachagua akasema.

Suala hilo la utathmini wa matokeo ya uchaguzi wa urais ni miongoni mwa ajenda zilizowasilishwa na mrengo wa Azimio na likakubaliwa kuwa miongoni mwa mambo yatakayoshughulikiwa na Kamati hiyo.

Kamati hiyo inaongozwa na Kiongozi wa Wengi Bunge Kimani Ichung’wah pamoja na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka anayewakilisha Azimio.

“Wakome kujadili matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2022. Waendelee kujadili ajenda zingine. Wazungumzie uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC, kuwekwa kwenye katiba Afisi ya Mkuu wa Mawaziri na ajenda nyinginezo,” Bw Gachagua akasisitiza akiongeza kuwa hakuna kipengele cha Katiba kinachoruhusu matokeo ya uchaguzi wa urais yakaguliwe upya baada ya mshindi kuthibitishwa.

“Mnamo Septemba 13, 2022, Rais William Ruto aliapishwa kuwa Rais. Mbona mnataka tuzungumzie uchaguzi tena?” akauliza.

Awali, Bw Gachagua amepinga vikali mazungumzo hayo yanayoendeshwa katika Bomas of Kenya akisema hayana maana yoyote na hayatazaa matunda yoyote.

“Naongea kama Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya nikisisitiza kwamba mazungumzo ya Bomas hayana maana yoyote na hakuna kitakachatokea huku. Raila alikutana na Rais na kujitafutia manufaa yake binafsi wale sio ya wenzake akiwemo Kalonzo,” Bw Gachagua akasema mnamo Agosti 23, 2023, akiwa katika eneo la Mwala, kaunti ya Machakos wakati wa mazishi ya mamake Mbunge wa eneo hilo Vincent Musyoka almaarufu Kawaya.

Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo inatarajiwa kupendekeza mageuzi ya kisheria na kisera kuhusu masuala yanayowaathiri Wakenya. Itafanya hivyo kwa kuheshimu Katiba na majukumu na hadhi ya asasi za kitaifa.

Miongoni mwa ajenda zilizowasilishwa na Kenya Kwanza ni; kuteuliwa upya kwa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kufanikishwa kwa sheria ya usawa wa kijinsia katika mabunge na asasi nyingine za serikali, kuwekwa kwenye Katiba kwa Afisi ya Mkuu wa Mawaziri na Sheria ya Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (CDF) na kuundwa kwa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani.

Nazo ajenda za Azimio ni pamoja na; Gharama ya Maisha, ukaguzi wa matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2022, uzingatiaji wa usawa katika uteuzi wa maafisa wa umma, serikali kukoma kuingilia uongozi wa vyama vya upinzani na uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC.

  • Tags

You can share this post!

LATA: Kundi la wasanii linalosaidia waraibu kuachana na...

Omanyala atetemesha kwenye mbio za mita 100 katika...

T L