• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 9:55 AM
Ubinafsi watajwa kiini cha viongozi kuhama kila mara

Ubinafsi watajwa kiini cha viongozi kuhama kila mara

NA WANDERI KAMAU

IMEBAINIKA kuwa lengo kuu la wanasiasa wengi wanaohama kutoka mrengo mmoja wa kisiasa hadi mwingine Uchaguzi Mkuu wa Agosti unapokaribia ni kujifaidi wao binafsi.

Ijapokuwa wengi wanatoa visingizio vya “kuwatetea raia” kama sababu kuu za kuhama kutoka mrengo mmoja hadi mwingine, lengo la wengi wao ni kuhakikisha kuwa hawatakuwa nje ya serikali baada ya uchaguzi huo.

Baadhi ya vigogo ambao wamekuwa wakionyesha kutapatapa kisiasa katika siku za hivi karibuni ni kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford-Kenya), magavana Alfred Mutua (Maendeleo Chap Chap), Amason Kingi (PAA), Peter Munya (Waziri wa Kilimo) kati ya wengine.

Licha ya Bw Musyoka kufika kwenye Jopo Maalum la Kumteua Mgombea-Mwenza wa Bw Raila Odinga katika muungano wa Azimio-One Kenya wiki mbili zilizopita, inaelezwa alichukua hatua hiyo baada ya kuraiwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Baada ya Bw Odinga kumteua kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua kama mgombea-mwenza wake, Bw Musyoka alitangaza atawania urais baada ya kukosa uteuzi huo.

KUKANGANYA

Bw Musyoka amekuwa akitoa misimamo ya kukanganya kupitia washirika wake wa karibu kama maseneta Enock Wambua (Kitui), Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na mbunge Dan Maanzo (Makueni).

“Nimemshikilia ndugu yangu Raila kwa muda mrefu. Tulianza kutembea naye safari yetu ya kisiasa tangu mwaka 2013. Ijapokuwa hatukufanikiwa 2013 na 2017, nina imani kwamba tunaingia Ikulu mwaka huu (2022),” akasema Bw Musyoka.

Msukumo wa kupata mgao wa serikali ndio unaotajwa kuwashinikiza Mabwana Mudavadi na Wetang’ula kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza, anaoongoza Naibu Rais William Ruto.

Kwa magavana Mutua (Machakos) na Kingi (Kilifi) mtawalia, waandani wao wanasema kuwa lengo lao ni kutengewa nyadhifa za uwaziri ikiwa mrengo wa Dkt Ruto utaibuka mshindi.

Wadadisi wanasema kuwa kabla ya Agosti, Wakenya watashuhudia wanasiasa wengi wakihama kutoka mrengo mmoja hadi mwingine, kwani misukumo yao mikuu ni jinsi watakavyofaidika.

Kulingana na mchanganuzi Dismus Mokua, huu ni wakati muhimu ambao wanasiasa hufanya maamuzi mazito ili kuepuka kuwa kwenye baridi ya kisiasa kwa miaka mitano.

“Bila shaka, wanasiasa wanaongozwa na kile watakachopata wao wenyewe na washirika wao. Hili limo vizuri kwenye mikataba ya kisiasa wanayotia saini. Wanalenga nyadhifa kama uwaziri, maspika wa bunge na seneti, makatibu wa wizara au usimamizi wa mashirika ya serikali,” akasema Bw Mokua.

MASLAHI

Kauli kama hiyo ndiyo anayotoa mdadisi James Yegon, anayesema kuwa sababu kuu ya vigogo wengi wa kisiasa kukosana ni kutozingatiwa kwa mikataba wanayoafikiana.

“Msingi wa siasa za sasa ni jinsi wanasiasa watakavyojifaidi kimaslahi kwa kujiunga na mrengo fulani wa kisiasa. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu kuu ya hayati Mwai Kibaki kukosana na Bw Odinga baada ya muungano wa Narc kuibuka mshindi kwenye uchaguzi wa 2002,” akasema Bw Yegon.

  • Tags

You can share this post!

UFUGAJI: Anazingatia mbinu bora kuwafuga ng’ombe wake

Wabunge wakataa vipengele kwenye mswada wa fedha...

T L