• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Uchaguzi wa Agosti 9 ulilenga kutimua waenezaji wa chuki za kikabila – Wetang’ula

Uchaguzi wa Agosti 9 ulilenga kutimua waenezaji wa chuki za kikabila – Wetang’ula

NA SAMMY WAWERU

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ametaja uchaguzi mkuu uliokamilika kama zoezi muhimu lililolenga kukomboa Kenya kutoka kwenye minyororo ya ukabila.

Akisifia baraza la mawaziri wa serikali ya Kenya Kwanza, walioteuliwa na Rais William Ruto, Bw Wetangula Jumapili alisema limesawazisha makabila yote nchini.

Mawaziri walioteuliwa hata hivyo hawajaidhinishwa na bunge, wakisubiri kupigwa msasa.

Akitetea matamshi yake, spika huyo mpya alisema usawa aliotaja unatokana na maamuzi ya Wakenya Agosti 9, 2022.

“Mwathiriwa mkuu katika uchaguzi uliokamilika alikuwa ukabila. Wakenya walipuuzilia mbali vitisho, na walioeneza ukabila wataishi na hiyo aibu hadi Yesu arudi,” Bw Wetangula akasema.

Alitoa kauli hiyo akizungumza katika Kaunti ya Uasin Gishu, hafla ya maombi kuridhia ushindi wa muungano wa Kenya Kwanza uchaguzini.

“Wakenya wamebadilika,” Wetangula akasisitiza.

Rais William Ruto ambaye ni kinara wa Kenya Kwanza alimenyana na mpinzani wake wa karibu, Bw Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance.

Dkt Ruto aliibuka mshindi, kesi ya kupinga matokeo ya kura iliyowasilishwa na Raila katika mahakama ya upeo ikifutiliwa mbali.

Waziri Mkuu huyo wa zamani alilalamikia udanganyifu kwenye uchaguzi mkuu.

  • Tags

You can share this post!

Urusi yaua watu 14 mjini Zaporizhzhia

Gachagua asimulia jinsi Ruto alivyopata umaarufu katika...

T L