• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Uhuru aanza kutoa Jubilee ICU

Uhuru aanza kutoa Jubilee ICU

NA CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa Jubilee wameanza kampeni kali za kukifufua chama hicho kote nchini baada ya hofu kuwa kingesambaratika kabisa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Ingawa wakereketwa wa chama hicho walishikilia kuwa kilikuwa imara, kilipata pigo baada ya Naibu Rais Willam Ruto na zaidi ya wabunge 100 kukihama na kuunda United Democratic Alliance (UDA).

Hatua hii ilidhoofisha chama hicho tawa – la na kufanya baadhi ya wanasiasa waliobaki waaminifu kutilia shaka uwezo wake wa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukamilisha muhula wake wa pili.

Hata hivyo, katika siku za hivi punde, chama hicho kimeonekana kupata nguvu mpya huku kikitarajiwa kuungana rasmi na ODM, pamoja na vyama vingine, chini ya mwavuli wa Azimio la Umoja wiki hii.

Kuanzia Februari 5, Rais Uhuru alipoongoza mkutano wa kundi la wabunge wa chama hicho (PG), wabunge na viongozi wengine wa chama hicho wamezidisha mikutano ya kukivumisha kuanzia ngazi za mashinani, hasa katika ngome yake ya Mlima Kenya.

Mnamo Ijumaa pekee, chama hicho kiliandaa mikutano katika kaunti za Nyeri, Murang’a, Nyandarua na Nakuru iliyowaleta pamoja viongozi wa matawi, wawaniaji viti mbalimbali na wanachama.

Katika Kaunti ya Murang’a, mikutano hiyo ilifanyika katika maeneo-bunge ya Kangema, Gatanga na Mathioya. Mkutano wa Nyandarua ulifanyika eneo-bunge la Kipipiri na kuongozwa na mbunge wa eneo hilo ambaye pia ndiye Kiongozi wa Wengi bungeni Amos Kimunya.

Kaunti ya Nakuru, mkutano wa kufufua Jubilee ulifanyika eneo-bunge la Njoro huku mikutano mingine ikipangwa kufanyika maeneo mengine wiki hii. Katika mikutano hiyo yote, wanachama na wakazi walihimizwa kuunga mkono kiongozi wa ODM, Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

Akiongea katika mkutano wa Nyeri, mbunge wa Kieni, Bw Kanini Kega alitangaza kuwa chama hicho “kimefufuka” na kiko tayari kudhamini wagombeaji katika nyadhifa zote isipokuwa wadhifa wa urais.

“Jubilee ingali imara na wale waliodhani kuwa chama hiki kimekufa wanaota ndoto

za mchana. Hatutadhamini mgombeaji wa urais, lakini tumeamua kusaka marafiki ambao tutafanya kazi nao. Tumeamua kwamba ni Raila tutakayemuunga mkono,” akasema.

“Hata hivyo, tutadhamini wagombeaji katika viti vyote vitano kuanzia udiwani hadi ugavana,” Bw Kega, mwenyekiti wa kamati ya bajeti bungeni, akaongeza.

Kilichojitokeza waziwazi katika mikutano hii ni kwamba Jubilee inarejesha ushawishi ambao ilikuwa nao kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017.

Hii ni baada ya chama hicho kupoteza wabunge na wanachama wengi kwa chama cha UDA kinachoongozwa na Dkt Ruto, aliyeongoza uasi baada ya Rais Kenyatta kuridhiana kisiasa na Bw Odinga mnamo Machi 9, 2018 kwa handisheki.

Naibu Rais na wabunge wandani wake walihisi kuwa muafaka huo ulilenga kuvuruga mipango ya awali ya Jubilee kuhusiana na urithi wa urais ambapo Rais Kenyatta aliahidi kumuunga mkono Dkt Ruto.

Jubilee ilianza kupoteza umaarufu tangu wakati huo hasa katika ngome zake za Mlima Kenya na Rift Valley ambapo wabunge wengi sasa wanaegemea UDA.

Hali hiyo ilidhihirika katika chaguzi ndogo za ubunge na udiwani ambazo zimefanyika tangu 2018 ambapo Jubilee ilibwagwa na vyama vichanga.

  • Tags

You can share this post!

Mawaziri watatu wa Joho wajiuzulu kuwania viti

Raila amgonga Ruto kwenye kampeni Pwani

T L