• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 9:49 AM
Uhuru abebe msalaba wa dhambi za Jubilee, Ruto asema akihojiwa

Uhuru abebe msalaba wa dhambi za Jubilee, Ruto asema akihojiwa

NA LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto amesema kuwa Rais Uhuru Kenyatta ndiye anastahili kubebeshwa lawama za serikali ya Jubilee.

Dkt Ruto aliwataka Wakenya kutomlaumu kwa ahadi na miradi ambayo serikali ya Jubilee ilishindwa kutekeleza.

Naibu wa Rais aliyekuwa akizungumza katika mahojiano na runinga ya NTV Jumapili usiku, alisema miradi yote aliyochangia ilifaulu.

“Kwa mfano, mikutano yote ya kujenga barabara ilikuwa ikifanyikia hapa ofisini kwangu hadi usiku wa manane. Tulikuwa tumeahidi kujenga kilomita 10,000 za barabara za lami.

“Mlisikia Rais katika hotuba yake ya Madaraka (Juni 1) akithibitisha kuwa tumejenga barabara za lami kilomita 11,000,” akasema Dkt Ruto.

Naibu wa Rais pia alisema kuwa uamuzi wa kuongeza idadi ya Wakenya wanaonufaika na umeme ulifanywa ofisini kwake.

Alisema uamuzi huo ulioafikiwa baada ya majadiliano ya ‘saa nyingi’ uliwezesha idadi ya Wakenya wanaonufaika na umeme kuongezeka hadi milioni 8.9 kutoka milioni 2.3.

Dkt Ruto pia alidai kuwa yeye ndiye alianzisha mpango wa kuhakikisha kuwa idadi kubwa ya vijana wanaokamilisha elimu ya sekondari wanajiunga na vyuo vya ufundi (TVET).

“Serikali ya Jubilee ilipoingia mamlakani mnamo 2013, idadi ya vijana waliokuwa TVET ilikuwa 89,000. Lakini sasa wamefikia karibu 500,000. Mpango huo umekuwa ukiendeshwa na ofisi yangu,” akadai Dkt Ruto.

Baada ya Jubilee kushinda muhula wa pili 2017, Dkt Ruto alisema, yeye na Rais Kenyatta waliafikiana kuanzisha miradi ya maendeleo ya Ajenda Nne; kuwezesha Kenya kuwa na chakula cha kutosha, huduma bora na nafuu za matibabu, makazi nafuu na ustawishaji wa viwanda.

“Lakini miradi hiyo yote ilisambaratika baada ya Rais kushirikiana na upinzani (Bw Raila Odinga. Hivyo, mimi nisilaumiwe,” akasema.

Naibu wa Rais amekuwa akishutumiwa kwa kutumia miradi ya serikali ya Jubilee kujipigia debe huku akijitenga na dosari zake kama vile kukolea kwa ufisadi serikalini na kupanda kwa gharama ya maisha.

Wakati huo huo, Naibu wa Rais alitetea hatua yake ya kuteua mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua kuwa mwaniaji mwenza wake huku akishikilia kuwa ana tajriba katika utumishi wa umma na amehitimu hata kuwa rais wa Kenya.

Katika mahojiano hayo, Dkt Ruto alisema kuwa atakubali matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

“Iwapo sitashinda uchaguzi wa Agosti, nitaenda nyumbani. Sasa nina wajukuu na nitaridhika tu kwani wadhifa wa Naibu Rais ambao nimewahi kushikilia si kitu kidogo,” akasema.

Alisema kuwa ametekeleza majukumu yake vyema akiwa Naibu wa Rais.

Licha ya Kifungu cha 23. (1) cha Sheria ya Uongozi na Maadili kuruhusu mawaziri kujihusisha na siasa, Dkt Ruto alisisitiza kuwa Mawaziri Fred Matiang’i (Usalama), Joe Mucheru (Teknolojia ya Mawasiliano) na Eugene Wamalwa (Ulinzi) wanakiuka sheria kwa kuunga mkono mpinzani wake mkuu Raila Odinga wa Azimio.

  • Tags

You can share this post!

Sakaja adai ana digrii

TUSIJE TUKASAHAU: Rais alikariri kuwa hatakubali hata inchi...

T L