• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 2:33 PM
Uhuru ajipanga asitikiswe na Karua Mlimani

Uhuru ajipanga asitikiswe na Karua Mlimani

NA MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta anaonekana kuweka mikakati ya kuhakikisha Jubilee inatamba eneo la Mlima Kenya katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ili asipoteze ubabe wa kisiasa ukanda huo kwa mgombeaji mwenza wa Azimio la Umoja One Kenya Martha Karua.

Rais Kenyatta ametawala siasa za Mlima Kenya tangu 2013 na nia yake ni kuendelea kudhibiti eneo hilo hata iwapo mgombea urais anayemuunga mkono Raila Odinga atapata ushindi au mpinzani wake Naibu Rais Dkt William Ruto.

Hatua ya Bw Odinga ya kumteua Bi Karua ilimweka kiongozi huyo wa Narc Kenya katika nafasi nzuri ya kumrithi Rais Kenyatta kama msemaji wa eneo la Mlima Kenya.

Lakini kiongozi wa nchi akiwa mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Azimio, amekuwa akitetea maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya kupitia Jubilee, iwapo Bw Odinga atatwaa uongozi wa nchi.

Viongozi wa Jubilee wamekuwa wakisema Bw Odinga atakuwa rais kwa muhula mmoja pekee na iwapo Rais Kenyatta bado atasalia kigogo wa siasa za Mlima Kenya, basi bado atakuwa na ushawishi kuhusu nani atakuwa rais mnamo 2027.

Tayari, Rais Kenyatta ameagiza washirika wake katika Jubilee kuhakikisha chama hicho kinashinda viti vingi kwenye uchaguzi ujao hatua ambayo itahakikisha ana usemi katika eneo la Mlima Kenya.

Akiwa na wabunge, maseneta na magavana wengi wa chama chake, Rais Kenyatta analenga kuendelea kuwa na usemi mkubwa hata ikiwa Bi Karua atakuwa naibu rais Azimio ikishinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Rais ametuamuru tuondoke afisini na tusitishe mikutano katika hoteli ili kuendeleza kampeni kabambe ya kuhakikisha Jubilee inashinda viti vingi Mlima Kenya,” akasema Mwenyekiti wa Jubilee Jeremiah Kioni.

Katibu huyo anasema kuwa wamefadhili wagombeaji maarufu katika kaunti za Nairobi, Nakuru, Nyandarua, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Nyeri, Embu, Meru, Tharaka Nithi na Laikipia.

Kulingana na wadadisi, Rais Kenyatta anataka kuhakikisha pia UDA haishindi viti vingi eneo la Mlima Kenya.

“Rais ametuambia kuwa ripoti za kijasusi anazopokea zinaonyesha kuwa Jubilee inaweza kuengua UDA kwa kutwaa viti vingi Mlima Kenya. Umaarufu wa UDA ulitokana na kuwa mwaniaji wake wa urais amekuwa akifanya kampeni kivyake mlimani kwa muda wa miaka tisa na sasa mambo yamebadilika kwa sasa,” akaongeza Bw Kioni.

Naye Gavana wa Kiambu James Nyoro anasema kuwa Rais Kenyatta anataka chama cha Jubilee kiwe dhabiti baada ya uchaguzi mkuu ujao ndipo hatima yake isiwe kama ya Narc na PNU ambazo zilikufa marehemu Rais Mwai Kibaki alipogombea kipindi cha pili na wakati alipoondoka uongozini mtawalia.

“Rais Kenyatta amewekeza rasilimali na juhudi kuhakikisha Jubilee inatwaa viti vingi Mlima Kenya. Ukanda wa Mlima Kenya unafaa kuwa na chama ambacho kinautambulisha kisiasa,” akasema Bw Nyoro.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu Ndung’u Gaithuma alisema kuwa washikadau wengi mlimani wamekutana na Rais Kenyatta na kupokezwa majukumu mbalimbali ya kuhakikisha kuwa wanapambana kutokomeza umaarufu wa UDA.

Naye Waziri wa zamani Peter Kenneth anasema kuwa Jubilee itapata mgao mkubwa ndani ya serikali ya Azimio la Umoja One Kenya iwapo itakuwa na idadi kubwa ya wabunge kwenye bunge lijalo.

  • Tags

You can share this post!

Obiri atawala 10,000m Kasarani, zamu ya Omanyala ni leo...

Wataalam sasa wataka wanafunzi wa umri wa miaka 15 kupatiwa...

T L