• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Umaskini wafaidi kampeni za vigogo

Umaskini wafaidi kampeni za vigogo

NA COLLINS OMULO

NAIBU Rais William Ruto na mwaniaji urais wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga wanatumia suala la umaskini kusaka kura kwa ahadi kuwa watasaidia walalahoi wakishinda.

Wataalamu wa uchumi wanasema ahadi za wawili hao kukabiliana na hali mbaya ya uchumi nchini ni mbinu tu ya kujitafutia kura kwani hawaelezi mbinu watakazotumia kutekeleza ahadi hizo.

Wanasiasa hao wanatumia umaskini na matatizo ya uchumi katika kampeni zao kutokana na kutambua mahangaiko wanayopitia wengi kutokana na mfumuko wa bei za bidhaa, ukosefu wa ajira, mfumo wa afya ulioporomoka, ukame miongoni mwa matatizo mengine tele.

Kura ya maoni iliyothaminiwa na kampuni ya Nation Media Group mapema Mei ilionyesha kuwa asilimia 75 ya Wakenya wana hofu zaidi kuhusu gharama ya juu ya maisha.

Takwimu nyingine zinaeleza kuwa idadi ya watu maskini nchini imeongezeka maradufu tangu 2014 huku matajiri wakitajirika zaidi na maskini wakizama zaidi katika uchochole, hivi kwamba kuna watu wawili ambao mali yao inatoshana na ya maskini milioni 16 wakiwa wamejumuishwa.

Dkt Ruto na Bw Odinga wamechukua fursa ya hali hiyo kubuni mikakati ya kampeni zao wakiwa na lengo la kushawishi wanyonge kuwaunga mkono.

WALALAHAI NA WALALAHOI

Dkt Ruto na muungano wake wa Kenya Kwanza wamekuwa wakichora picha ya uchaguzi wa mwaka huu kuonekana kuwa ni ushindani kati ya “walalahai” na “walalahoi” kwa kueleza kuwa Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wanawakilisha walalahai dhidi ya mwananchi wa kawaida.

Azimio la Umoja nao wanajiuza kama wanamageuzi ambao wana suluhu kwa matatizo mengi ya kiuchumi nchini.

Kulingana na msomi wa sayansi ya siasa na usimamizi, Prof Winnie Mitulla, ongezeko la bei za bidhaa muhimu na hali duni ya uchumi ni miongoni mwa masuala makuu ambayo yatatumiwa na wanasiasa kusaka kura mwaka huu 2022.

Prof Mitulla anasema Dkt Ruto na Bw Odinga wametoa ahadi za kuinua walalahoi kimaisha, lakini hawasemi jinsi watakavyoafikia hayo: “Mgombeaji anaposema atafufua uchumi na kuboresha maisha ya wananchi ni lazima pia afafanue jinsi atakavyofanya hivyo na vile manufaa hayo yatamfikia mwananchi mashinani.”

Anasema hakuna tofauti kati ya mpango wa Ruto wa maendeleo kuanzia mashinani pamoja na ule wa Azimio wa kusaidia wanyonge katika jamii, akieleza kuwa wote wanalenga kundi sawa la wapiga kura.

“Kile wote wanasema ni kimoja. Hata hivyo, ahadi hizo zinaelezwa kisiasa tu bila kufafanuua mpango wa kuzitekeleza. Wanapasa kutwambia vile watatimiza ahadi hizo,” aeleza.

Msomi wa sayansi ya jamii, Prof Maurice Amutabi anakubaliana na kauli hiyo akisema katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022 wapigakura wanaangazia walio na suluhisho kwa matatizo ya kiuchumi, elimu, hali mbaya ya kibiashara, ukosefu nwa ajira na changamoto nyinginezo.

Prof Amutabi anasema Azimio na Kenya Kwanza wametambua masuala yanayowahangaisha Wakenya, ndiposa wanasuka kampeni zao kwa ahadi za kuwapa matumaini wananchi wanaohangaika.

“Kinyume na awali ambapo ukabila ulikuwa suala kuu la uchaguzi, wakati huu suala la uchumi lina umuhimu mkubwa zaidi. Mwaniaji atakayethibitisha kuwa na mpango na uwezo wa kuboresha hali ya maisha ndiye ataungwa mkono na wengi,” asema Mbunge wa Kitui ya Kati, Dkt Makali Mulu, ambaye pia ni mwanauchumi.

Katika kushawishi hisia za maskini, Dkt Ruto amebuni jopo la wataalamu wa uchumi kuandika mwongozo wa kiuchumi anaoahidi atatekeleza iwapo Wakenya watamchagua.

Muungano wa Azimio pia umezindua mpango wake wa uchumi ukilenga kusaidia walalahoi pamoja na kuwekeza katika uzalishaji wa chakula na kuboresha afya kwa wote.

Lakini kulingana na Dkt Mulu, mipango ya Dkt Ruto na Bw Odinga inaonekana kuwa ahadi hewa kwani hakuna anayeeleza kwa kina jinsi ya kuifadhili ikizingatiwa hali ngumu ya uchumi inayokumba Kenya hasa kutokana na deni kubwa la kitaifa.

“Wanapiga domo sana kuhusu yale watawafanyia Wakenya, lakini hawaelezi mipango hiyo itatekelezwa vipi kifedha. Nyingi ya ahadi wanazopeana hazitatekelezwa,” aeleza Dkt Mulu.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru, Raila waomboleza kifo cha mbunge wa Rabai

TALANTA YANGU: Mjuzi wa saksafoni

T L