• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Usawa Kwa Wote Party chaendelea kusajili wanachama wake

Usawa Kwa Wote Party chaendelea kusajili wanachama wake

Na LAWRENCE ONGARO

CHAMA cha Usawa kwa Wote, kimezindua mpango wa kuhamasisha vijana kote nchini kwa lengo la kukiimarisha.

Chama hicho cha Gavana wa Murang’a Mwangi Wa Iria, kimezindua kikundi cha Usawa Youth Volunteers, ambacho kimeanza shughuli ya kusajili wanachama kutoka kaunti zote 47 za nchi.

Afisa mmoja wa Usawa Kwa Wote Party Bw James Mwangi, alieleza kuwa chama hicho kinafanya mikakati ili kuimarika katika pembe zote za nchi.

“Tunataka kuona ya kwamba chama chetu kinajulikana kote nchini ili ifikapo wakati wa uchaguzi kiwe na ushawishi na kuvutia wafuasi,” alisema Bw Mwangi.

Alisema chama hicho kinatarajia kuwahamasisha vijana kote nchini ili waweze kuwa na mpangilio wa kimaisha.

Alieleza kuwa asilimia 70 ya vijana hapa nchini wamekosa nafasi mwafaka ya kujiendeleza na kwa hivyo chama hicho kinafanya mikakati kuwainua.

Aliyasema hayo Alhamisi katika mkahawa mmoja mjini Thika ambapo vijana zaidi ya 1000 walisajiliwa ili kuendelea na mpango huo katika kaunti nyinginezo.

Chama hicho kinalenga kusajili vijana wapatao 4 milioni kote nchini ili kuwatafutia nafasi waweze kujiendeleza kimaisha.

Bw Kangacha Kariethe ambaye ni mmojawapo wa vijana wanaosajili wengine, alisema wakati huu vijana kutoka eneo la Mlima Kenya hawatakubali kutumiwa vibaya na wanasiasa.

“Sisi kama vijana tutafuata viongozi ambao nia yao ni kuinua maslahi ya kila mmoja nchini. Siasa za kupewa pesa ili kupigia viongozi kura hatutazifuata tena,” alisema Bw Kariethe.

Naye kiongozi wa vijana kutoka Mlima Kenya Bw Martin Kimundia, alisema wao kama vijana watahakikisha chama cha Usawa Kwa Wote kimepata ushawishi si tu katika eneo hilo lakini nchini kote.

Alisema kwa wakati huu chama hicho kimeshika mizizi katika kaunti za Murang’a, Nyeri, na hata Nairobi.

Alisema wakati huu “tunataka teknolijia mpya ili kuenda sambamba na matakwa ya wananchi.”

Aliwashauri viongozi wote wanaotaka uongozi kuja na sera zitakazowanufaisha wananchi lakini wasilete porojo kwa wananchi.

Kwa kauli moja vijana waliofika kwenye hafla hiyo walisema huu utakuwa mwamko mpya kwa sababu watawachagua viongozi wenye maono wala sio wenye kuleta porojo.

You can share this post!

Cristiano Ronaldo aongoza kwa umaarufu kwenye Instagram

Itakuwa moto Italia, Ubelgiji zikikwaruzana robo ya Euro...