• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wabunge wa Azimio waliokwepa kura au kuunga mkono Mswada wa Fedha kuadhibiwa

Wabunge wa Azimio waliokwepa kura au kuunga mkono Mswada wa Fedha kuadhibiwa

NA CHARLES WASONGA

KUPITISHWA kwa Mswada wa Fedha wa 2023 Jumatano usiku kumesababisha joto katika kambi ya Azimio huku chama cha ODM kikitisha kuadhibu wabunge waliokosa kufika Bungeni kupinga mswada huo.

Aidha, duru zinasema kuwa uongozi wa Azimio umeitisha mkutano kujadili suala hilo huku mswada huo ukitarajiwa kusomwa kwa awamu ya tatu Bungeni wiki ijayo.

Viongozi wa Azimio wamewalaumu wabunge wao ambao walipiga kura ya NDIO au walikwepa kushiriki shughuli hiyo, hali iliyochangia mswada huo kupita awamu ya pili kwa kupigiwa kura na jumla ya wabunge 176.

Ni wabunge 81 pekee waliopiga kura ya LA katika shughuli hiyo iliyoshirikisha jumla ya wabunge 257. Hii ina maana kuwa jumla ya wabunge 92 kutoka mirengo yote miwili, Azimio na Kenya Kwanza, hawakuwa Bungeni kupiga kura.

Chama cha ODM kimewaandikia barua wabunge wake 28 ambao ama walipiga kura ya kuunga mkono mswada huo au hawakuwa Bungeni wakati wa upigaji kura.

Kwenye barua hiyo ambayo iliandikwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna, wabunge hao wamepewa muda wa saa 48 kuelezea ni kwa nini wasiadhibiwe kwa mujibu wa kanuni za chama hicho kwa kwenda kinyume na msimamo wake wakati wa upigaji kura.

“Kulingana na kanuni za adhabu za ODM, wabunge waliotajwa wametumiwa barua wakitakiwa kujitetea kwa kukiuka msimamo wa chama kuhusu suala la Mswada wa Fedha,” inasema barua hiyo iliyoandikwa na Bw Sifuna ambaye pia ni Seneta wa Nairobi.

Miongoni mwa wabunge wanaotarajiwa kuadhibiwa na ODM ni Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nairobi Esther Passaris, Elisha Odhiambo (Gem), Babu Owino (Embakasi Mashariki), Adow Mohammed (Wajir Kusini) na Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi.

Wengine ambao walikuwa Bungeni lakini hawakushiriki upigaji kura walikuwa ni Gideon Ochanda (Bondo) na Otiende Amollo (Rarieda).

Wabunge wa ODM ambao hawakuwepo Bungeni lakini hawataadhibiwa ni wale ambao wamezimwa kuhudhuria vikao vya bunge kwa wiki moja kwa kushiriki vurugu wiki jana ambapo Mbunge Maalum Sabina Chege alijeruhiwa kidole. Wao ni pamoja na; Rosa Buyu (Kisumu Magharibi), T.J Kajwang’ (Ruaraka), Millie Odhiambo (Suba Kusini), Amina Mnyazi (Malindi) na Catherine Omanyo (Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Busia).

Baadhi ya wabunge wa Azimio na ODM ambao walikosa kushiriki upigaji kura kuhusu Mswada wa Fedha wa 2023 walijitetea wakisema kuwa hawakuwa na habari kwamba shughuli hiyo ingeendeshwa Jumatano usiku.

Bw Amollo alimlaumu Spika Moses Wetang’ula kwa kile alichosema ni kuwahadaa kuwa mswada huo ungepigiwa kura Jumanne, Juni 20, 2023.

“Kwenye agizo lake wiki jana, Spika alisema kuwa mswada huo ungejadiliwa Jumatano na Alhamisi kisha upigiwe kura Jumanne juma lijalo,” akasema mbunge huyo Alhamisi baada ya kuungana na wenzake kuondoka Bungeni punde tu Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u alipoanza kusoma makadirio ya bajeti.

Naye Babu Owino alijitetea kwamba alienda kujiandaa kwa kesi ambapo ameshtakiwa kumjeruhi kwa risasa DJ Evolve.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba wabunge wote wa Azimio ambao walipiga kura ya NDIO na wale ambao walikwepa kuhudhuria vikao vya Bunge mnamo Jumatano, waliondolewa kutoka makundi yote – ya mtandao wa WhatsApp – ya upinzani na hata lile la Kundi la Wabunge (PG).

Azimio ilikerwa zaidi na dai la kiranja wa wengi Silvanus Osoro kwamba kutokuwepo kwa baadhi ya wabunge wa upinzani kulikuwa ni sehemu ya njama ya Kenya Kwanza kuhakikisha kuwa mswada huo unapita hatua hiyo ya pili.

“Umegundua kuwa idadi kubwa ya wabunge wa upinzani hawakuwepo ukumbini. Huu ni mchezo, ni mchezo ambao tulicheza. Tuliwashawishi na tukasababisha wasihudhurie. Ni mbinu ambayo tulibuni kuhakikisha kuwa tunapitisha yale yenye manufaa kwetu kama Kenya Kwanza,” Osoro akasema kwenye kanda ya video inayosambaa mitandaoni.

Saa chache kabla ya mswada huo kujadiliwa na kupigiwa kura, mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Azimio Wycliffe Oparanya alihutubia kikao cha wanahabari na kuwataka wabunge wa Azimio kuangusha mswada ambao umeshutumiwa kwa kupendekeza nyongeza ya ushuru.

“Wabunge wetu wameshauriwa kufika Bungeni kwa wingi na kuhakikisha kuwa wamepinga Mswada huo wa Fedha. Wameagizwa kukataa mswada huo unaolenga kukandamiza,” Oparanya akasema Jumatano asubuhi.

Duru zinasema kuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga ameitisha mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho kujadili masuala kadhaa ambapo mojawapo ya masuala hayo ni mienendo ya wabunge wake wakati wa upigaji kura kuhusu Mswada wa Fedha.

Wabunge wengine wa Azimio ambao walikosa kupiga kura ni pamoja na; Mark Nyamita (Uriri, ODM), Walter Owino (Awendo, ODM), Titus Lotee (Kacheliba, ODM), Farah Maalim (Dadaab, Wiper), Peter Nabulindo (Matungu, ODM), Felix Odiwuor (Jalang’o, ODM), Fabian Mule (Kangundo, Wiper), miongoni mwa wengine.

  • Tags

You can share this post!

Shule ya hadhi yatelekezwa kwa kuwa kwenye mpaka wa...

Utajuaje familia yenye mshikamano na ushirikiano mzuri?

T L