• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wabunge wangu wataangusha mswada – Ruto

Wabunge wangu wataangusha mswada – Ruto

Na WAANDISHI WETU

NAIBU Rais William Ruto amesema kwamba, wabunge wanaomuunga mkono wataendelea kuvuruga Mswada wa Vyama vya Kisiasa, unaopangiwa kuendelea kujadiliwa kwa siku tatu wiki ijayo.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ameita kikao maalum cha bunge kuanzia Januari 5 hadi 7 mwaka huu 2022 kujadili mswada huo.

Matamshi yake yalionekana kulenga kushambulia azimio la mkutano wa Bukhungu II ambapo kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, aliidhinishwa na baadhi ya viongozi wa Magharibi mwa Kenya.

Mkutano huo uliandaniwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli.

Dkt Ruto alisisitiza kuwa Wakenya wanafaa kuruhusiwa kuchagua wanayemtaka na sio kuamuliwa na watu wachache wanaokutana faraghani.

Dkt Ruto alisema bila muafaka kuhusu Mswada wa Vyama vya kisiasa, washirika wake bungeni wataendelea kuhujumu mchakato wa kuupitisha.

Alipuuza wabunge wanaounga Azimio la Umoja la Bw Odinga kwa kudai wako na idadi kubwa ya wabunge akisema kwamba mrengo wake sasa uko na zaidi ya wabunge 134 ambao wako tayari kukabiliana na waandalizi wa Mswada huo.

“Wale tunaoshindana nao walijaribu kututisha tupeleke wabunge, tulipeleka wabunge 134 na ajenda yao haikuweza kupita na ikaahirishwa, Mswada huo utakaporejeshwa, tutaketi na kuhujumu tena wakiendelea kujigamba,” alisema Dkt Ruto.

Alishikilia kuwa kipengele kinachofupisha muda wa kuunda miungano ya kisiasa kinanuiwa kulazimisha vinara wa One Kenya Alliance (OKA) kufichua mikakati yao ya kisiasa mwezi huu wa Januari.

  • Tags

You can share this post!

Rice kuwa nahodha mpya wa West Ham baada ya Noble kustaafu...

Jinsi wakazi wa Nairobi walivyokaribisha mwaka mpya

T L