• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Jinsi wakazi wa Nairobi walivyokaribisha mwaka mpya

Jinsi wakazi wa Nairobi walivyokaribisha mwaka mpya

Na SAMMY WAWERU

MWAKA mpya wa 2022 ulikaribishwa kwa staili, baadhi wakikongamana katika maeneo ya kuabudu, burudani, baa na barabarani.

Kinyume na miaka ya awali, ambapo idadi kubwa hulaki mwaka mpya kanisani na katika maeneo ya burudani, 2022 wengi walilazimika kusalia nyumbani.

Hatua hiyo ilichangiwa na kanuni na mikakati kuzuia msambao wa ugonjwa wa Covid-19, iliyopendekezwa na Wizara ya Afya (MoH).

Hata ingawa mwishoni mwa 2021 serikali ililegeza kamba sheria hizo, inaendelea kuhimiza wananchi kuzizingatia.

Himizo hilo linatokana na kuendelea kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona, Kenya ikithibitisha kuwa mwenyeji wa kirusi hatari cha Omicron na ambacho madaktari na wanasayansi wanaonya kinasambaa kwa kasi.

Mitaa mbalimbali Kaunti ya Nairobi, wengi wa wakazi hawakuwa na budi kuukaribisha mwaka mpya kwa kufuatilia vipindi vya mahubiri kwenye runinga zilizovipeperusha moja kwa moja.

Kwa mfano, katika mtaa wa Zimmerman wale ambao hawakujumuika katika maeneo ya kuabudu au burudani, mshale wa kronomita ya saa ulipogonga saa sita kamili Jumamosi, walitumia veranda na vilele vya ghorofa wanazoishi kulaki 2022.

“Mwaka wa 2021 na 2022, yote miwili niliilaki nikiwa kwenye nyumba. Corona ilibadilisha mkondo wa maisha,” Dennis Njoroge, mkazi wa Carwash akaambia Taifa Leo.

Sauti za furaha na fataki zilihanikiza kote, kuanzia Kasarani, Mwiki, Githurai, Kahawa West, sawa na mitaa mingine.

Baadhi ya wahudumu wa bodaboda walizunguka kwa muda wa dakika thelathini hivi wakipiga honi, ishara ya kuridhia mwaka mpya.

“Mwaka uliopita ulikuwa mgumu na tunatumai 2022 ni mwaka unaokuja na baraka,” mhudumu wa bodaboda Bw Mwangi Desire akasema.

Ijumaa, Desemba 31 kabla jua kutua, barabara ya Karii, inayounganisha Thika Super Highway na Kamiti Road, shughuli za usafiri na uchukuzi ziliendelea kama kawaida, watu wakitoka kazini.

Wakati wa kukaribisha 2022, magari kadha yalionekana barabarani pengine wamiliki au madereva wakitoka kazini ama maeneo ya burudani kujienjoi.

Kwenye hotuba yake kwa taifa kuufunga mwaka na kukaribisha mgeni, Rais Uhuru Kenyatta aliwatakia Wakenya heri njema.

“Kwa waliohangaika 2021 na kukadiria hasara, mwaka wa 2022 utakuwa wenye baraka na uponyaji,” Rasi Kenyatta akasema.

Katika risala zake za heri njema, kiongozi wa nchi alitumia jukwaa hilo kuelezea miradi ya maendeleo aliyotekeleza kipindi cha miaka tisa iliyopita, na anayotarajia kuafikia akielekea kustaafu.

Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu, viongozi na wanasiasa wanaomezea mate viti mbalimbali vya kisiasa 2021 wakiandaa jukwaa la kampeni.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wangu wataangusha mswada – Ruto

Wanajeshi 4 wa Tanzania wajeruhiwa

T L