• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Wafuasi wa Kenya Kwanza, Azimio wazua fujo jiji kuu

Wafuasi wa Kenya Kwanza, Azimio wazua fujo jiji kuu

NA WANDERI KAMAU

KIZAAZAA kilizuka Jumapili jijini Nairobi, baada ya makundi yanayounga mkono miungano ya kisiasa ya Azimio-One Kenya na Kenya Kwanza kukabiliana vikali katika Uwanja wa Jacaranda, ulio eneobunge la Embakasi Mashariki.

Nusura kizaazaa hicho kivuruge mkutano wa Naibu Rais Willam Ruto, uliofanyika baadaye katika uwanja huo, japo chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Kizaazaa hicho kilianza Jumapili asubuhi, baada ya vijana wanaounga mkono mbunge wa eneo hilo, Babu Owino, kufika katika uwanja huo na kushikilia kwamba alikuwa ashapata kibali cha kuandaa mkutano wake katika uwanja huo.

Kwenye taarifa, Bw Owino alidai alipata kibali cha kuandaa mkutano huo Alhamisi, baada ya kulipa ada ya kuandaa mkutano huo kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Hata hivyo, mwaniaji ubunge katika eneo hilo kwa tiketi ya UDA, Bw Francis Mureithi, alisema alipata kibali cha kuandaa mkutano huo kutoka kwa serikali ya Kaunti, baada ya kulipa ada ya Sh30,000 mnamo Jumatano.

Kwenye taarifa yake, aliambatanisha risiti aliyodai ilikuwa ithibati ya kupata kibali cha kuandaa mkutano huo.

Lakini katika kile kilichoonekana kuwa hatua ya kuzima makabiliano yoyote ambayo yangeweza kutokea, polisi walifika mapema katika uwanja huo na kuzuia makundi kutoka pande zote mbili kufika uwanjani.

Licha ya uwepo wa polisi, makundi hayo mawili yalijaribu kuingia kwa nguvu, hali iliyowalazimu kutumia vitoa machozi ili kuyatawanya makundi ya vijana yaliyokuwa yamefika katika kiingilio kikuu cha uwanja huo.

Kwenye patashika iliyozuka, Bw Mureithi alijeruhiwa kichwani baada ya kurushiwa jiwe, akiwalaumu wafuasi wa Bw Owino. Watu wengine wawili pia walijeruhiwa.

Polisi waliondoka mwendo wa saa tano, baada ya kurejesha hali ya utulivu na kuruhusu kambi ya Dkt Ruto kuendelea na mkutano huo. Mtu mmoja pia alikamatwa kwa kuzua ghasia.

Kufuatia kizaazaa hicho, Dkt Ruto aliwakashifu baadhi ya maafisa wakuu serikalini, akisema wamekuwa wakifanya kila juhudi kuzima na kuvuruga kampeni za muungano wa Kenya Kwanza bila mafanikio.

Akihutubu awali katika Kanisa la Jesus Winner Ministries, eneo la Roysambu, Kasarani, Dkt Ruto alidai kuwa washindani wao waliharibu jukwaa walilokuwa wameweka katika uwanja huo Jumamosi usiku “kwa kuogopa umaarufu wao.”

“Waliharibu hata jukwaa letu ili kuvuruga mkutano wetu. Hata hivyo, hatutatishika hata kidogo. Wana siku chache sana kuendeleza vitisho vyao,” akasema Dkt Ruto.

Mgombea-mwenza wa Dkt Ruto, Bw Rigathi Gachagua, aliwataja Katibu wa Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho na Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Nairobi, Bw Kang’ethe Thuku, kuwa “wapangaji njama wakuu kuvuruga mkutano wao.”

“Ningetaka kuwashauri Dkt Kibicho na Bw Thuku kukoma kutumika vibaya na washindani wetu. Wana siku 50 pekee ofisini. Badala ya kutumika vibaya, wanapaswa kuwa wakipanga vitu vyao ili kuondoka ofisini,” akasema Bw Gachagua.

Kwenye taarifa, Katibu Mkuu wa UDA, Bi Veronicah Maina, alimrai Inspekta Jenerali wa Polisi, Hillary Mutyambai kufanya kikao na vyama vya kisiasa kuhusu uzingatiaji wa amani kwenye kampeni za uchaguzi.

Hadi tukienda mitamboni Jumapili, muungano wa Azimio haukuwa umetoa taarifa yoyote kuhusu suala hilo.

  • Tags

You can share this post!

Presha katika ODM kuzuia wafuasi kususia uchaguzi

KINYANG’ANYIRO 2022: Kaunti ya Homa Bay

T L