• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Presha katika ODM kuzuia wafuasi kususia uchaguzi

Presha katika ODM kuzuia wafuasi kususia uchaguzi

MAUREEN ONGALA NA WINNIE ATIENO

VIONGOZI wa chama cha ODM katika eneo la Pwani, sasa wameanzisha kampeni ya kuhimiza wafuasi wao kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Katika mikutano mbalimbali ya kisiasa ambayo imefanyika siku za hivi majuzi, wanasiasa hao wameonekana wakisisitiza sana kuhusu hitaji la wafuasi kushiriki katika uchaguzi huo ili kumhakikishia kinara wao, Bw Raila Odinga, ushindi.

Baada ya kura za mchujo wa wagombeaji ambapo baadhi ya wanachama walilalamikia jinsi baadhi ya tikiti zilivyotolewa moja kwa moja, wadadisi wa kisiasa walikuwa wameonya kuwa huenda wafuasi wa wale waliokosa tikiti wakakosa kujitokeza uchaguzini.

Ilihofiwa hatua hiyo ingeathiri kura za urais ambazo zingeingia katika kapu la Bw Odinga, anayewania chini ya chama cha kisiasa cha Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Mbunge wa Kilifi Kusini, Bw Ken Chonga, alisema Bw Odinga kwa sasa amepiga hatua kubwa kukaribia kupata ushindi wa urais lakini mafanikio yake yanategemea zaidi wafuasi wake kujitokeza ifikapo Agosti 9.

“Tunapozungumza mguu mmoja wa Raila uko katika ikulu Nairobi, na kwa sasa ni kwetu sisi kumpigia kura na kumchagua Agosti 9, ili aweze kupita kura na kuendeleza malengo yake ya maendeleo kwa Wakenya,” akasema Bw Chonga.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Jilore, eneobunge la Malindi, mbunge huyo alisema kuna matumaini uongozi wa Bw Odinga utatatua changamoto ambazo Wakenya wamepitia kwa muda mrefu.

Mgombeaji ugavana kwa tikiti ya ODM eneo la Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, alipigia debe upigaji kura kwa wagombeaji wote wa ODM akisema njia hiyo ndiyo itakayomsaidia Bw Odinga kuendesha serikali vyema endapo atashinda urais.

Wanasiasa hao walitumia mikutano yao pia kuhamasisha umma kuhusu manifesto ya urais ya Azimio inayojumuisha masuala ya kuboresha usimamizi wa sekta za kibiashara zinazotegemea bahari, marekebisho ya sheria zinazosimaimia bandari za nchi, ufufuzi wa utalii, utatuzi wa changamoto za umiliki wa ardhi miongoni mwa mengine.

Katika Kaunti ya Mombasa, Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, na mwenzake wa Jomvu, Bw Badi Twalib, waliwarai wafuasi wa ODM kuthibitisha kuwa maelezo yao yote ya kupiga kura yako sawa katika vituo ambapo walijisajili kupigia kura, kabla ya Agosti 9.

Bw Nassir alieleza hofu kwamba utata unaoendelea katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuhusu watu kuhamishwa kutoka kwa vituo ambapo walijisajili huenda ukaathiri idadi ya kura za urais zinazotarajiwa na chama hicho kwa Bw Odinga.

“Mnaweza kuthibitisha kama nyinyi ni wapigakura kwa kutuma ujumbe mfupi kwa simu za rununu ili mjue mahali ambapo kura zenu ziko ama mahali mtakapotakikana kupiga kura. Nimeskia watu wengi wametolewa katika kituo cha karibu na hatuwezi kukubali hilo lifanywe kwa njia haramu kwa sababu hii ni ngome ya ODM,” akasema Bw Nassir.

Alitaka IEBC ihakikishe kuwa, kama kuna watu waliohamishwa kwa njia haramu hatua zichukuliwe mara moja ili kuwe na haki katika uchaguzi.

Bw Odinga anajitahidi kuthibiti ngome zake za Pwani dhidi ya ushindani kutoka kwa mpinzani wake wa karibu katika uchaguzi wa urais, Naibu Rais William Ruto, ambaye anawania kiti hicho kupitia Chama cha UDA kilicho ndani ya Muungano wa Kenya Kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Wawaniaji walilia IEBC wakidai serikali ya Joho...

Wafuasi wa Kenya Kwanza, Azimio wazua fujo jiji kuu

T L