• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
Wanaotaka kumrithi Uhuru wafuatilia hotuba yake bungeni

Wanaotaka kumrithi Uhuru wafuatilia hotuba yake bungeni

Na CHARLES WASONGA

WANASIASA ambao wanamezea mate kiti cha Rais Uhuru Kenyatta akistaafu mwaka 2022, jana Jumanne walifika bungeni kufuatilia hotuba yake kuhusu Hali ya Taifa ishara kwamba wanajiandaa kwa wadhifa huo.

Kando na Naibu Rais William Ruto ambaye, kikatiba ni msaidizi mkuu wa Rais Kenyatta na hangekosa kikao hicho, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga alifika mapema katika majengo ya bunge kufuatilia hotuba hiyo.

Vile vile, walikuwepo vinara wanne wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA); Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

Wote hao isipokuwa Bw Wetang’ula wameidhinishwa rasmi na vyama vyao kuwania urais 2022.

Japo Bw Odinga, ambaye ni kiongozi wa ODM hajatangaza rasmi kuwa atawania urais, amekuwa akiendesha kampeni kote nchini chini ya kauli mbiu ya Azimio la Umoja, akijinadi kama kiongozi anayefaa kumrithi Rais Kenyatta.

Mwanasiasa huyo mkongwe ameandaa mkutano mkubwa katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Nairobi mnamo Desemba 10, 2021 ambapo anatarajiwa kutangaza rasmi azma yake.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, ambaye pamoja na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka walioongoza kikao hicho, pia ametangaza kuwa atawania urais kwa tiketi ya chama cha Democratic Party (DP).

Joto la siasa za urithi wa Rais Kenyatta lilishamiri bungeni Spika Muturi aliwatambua rasmi vigogo hao kwani wabunge wandani wao waliwashangilia kwa sauti za juu majina yao yalipotajwa.

You can share this post!

MAKAVAZI CUP: Omariba, Sakawa waibuka mabingwa wa vishale

Mwaura arejea rasmi kama Seneta Maalum

T L