• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:10 AM
Wanasiasa wa UDA North Rift waelezea matumaini ya uchaguzi huru

Wanasiasa wa UDA North Rift waelezea matumaini ya uchaguzi huru

NA TITUS OMINDE

WANASIASA wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kutoka North Rift wamewahakikishia wafuasi wao kuwa uchaguzi wa viongozi wa mashinani wa chama hicho ambao utafanyika Desemba 9, 2023, utakuwa wazi na huru.

Walikuwa wakizungumza wakati wa mkutano wa viongozi wa chama hicho kutoka Rift Valley ambao ulifanyika katika kituo cha Fanyika Homecraft eneo la Pioneer mjini Eldoret.

Wanasiasa hao waliongozwa na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi na mbunge maalum Joseph Wainaina.

“Uchaguzi ujao wa viongozi wa mashinani utakuwa huru na wa haki. Wagombea wote wanaowania viti mbalimbali hawafai kuogopa bali wazingatie mahitaji yote kabla ya uchaguzi,” akasema Bw Sudi.

Bw Sudi alikariri kuwa uchaguzi huo utadumisha maadili ya chama kuhusu demokrasia na uwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Matamshi ya Bw Sudi yalikusudiwa kuimarisha uanachama wa UDA na kukumbatia dhamira isiyoyumbayumba katika ufufuaji wa uchumi na kanuni za kidemokrasia chamani.

Wanasiasa hao walitumia mkutano huo kuwasihi Wakenya kuwa na subira huku serikali ya Kenya Kwanza ikiendelea kutafuta mbinu za kukabili changamoto za kiuchumi zinazowaumiza Wakenya.

“Tunawahimiza Wakenya kuwa na subira zaidi kwa Rais William Ruto. Kama viongozi, tunaamini katika uwezo wake wa kuimarisha uchumi ifikapo mwaka 2024,” akasema Bw Wainaina.

Bw Wainaina alielezea matumaini katika hatua zilizochukuliwa na Rais Ruto kuelekea kufufua uchumi.

Bw Wainaina alisema ana matumaini kuwa mpango wa kina wa kiuchumi wa kiongozi wa nchi utatoa matokeo madhubuti kufikia mwaka 2024. Mbunge huyo alisema Rais Ruto ana sera zitakazochochea ukuaji wa uchumi na kupunguza matatizo ya kifedha yanayowakabili Wakenya wengi.

“Kenya itakuwa miongoni mwa nchi zilizoendelea zaidi barani Afrika,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa watano wa wizi wa Sh94 milioni za Quickmart...

Mwago sasa adai baadhi ya machifu Starehe ni...

T L