• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Wanasiasa wazimwa kushiriki harambee kuanzia Desemba 9

Wanasiasa wazimwa kushiriki harambee kuanzia Desemba 9

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto na wanasiasa wengine wanaomezea mate viti katika uchaguzi mkuu ujao wamepata pigo baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwazima kushiriki hafla za kuchanga fedha.

Akiongea alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Masuala ya Sheria, mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati alionya kwamba mgombeaji yeyote atakayevunja amri hiyo atazuiwa kushiriki uchaguzi mkuu wa 2022.

“Mwanasiasa yeyote anayetaka kuwania kiti katika uchaguzi mkuu ujao hapaswi kushiriki katika harambee baada ya Desemba 9, 2021. Kufanya hivyo kutakuwa sawa na kukiuka sheria za uchaguzi na mwanasiasa kama huyo hataruhusiwa kushiriki uchaguzi mkuu ujao,” akasema Bw Chebukati.

Amri ya IEBC inatokana na sehemu ya 26 ya Sheria ya Uchaguzi inayosema kuwa mtu anaweza kuzuiwa kushiriki katika uchaguzi ikiwa atashiriki kwa njia yoyote katika hafla ya mchango wa fedha ndani ya miezi minane kabla ya tarehe ya uchaguzi huo au wakati wa uchaguzi huo.

Sehemu ya 26 (1) ya sheria hiyo inasema pia inapiga marufuku hatua ya mtu fulani kumchangia fedha mwanasiasa anayegombea wadhifa wowote chini ya sheria hiyo.

“Kwa hivyo, kulingana na shera hiyo wawaniaji hawawezi kushirika michango ya fedha moja kwa moja au kupitia washirika wao ndani ya miezi minane kabla ya uchaguzi mkuu,” Bw Chebukati akawaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na Seneta wa Nyamira Okong’o O’Mogeni.

“Hii itazuia mienendo ya wawaniaji kuwashawishi wapigakura kwa kuchangisha fedha za kuwasaidia (raia hao) kwa njia mbalimbali,” mwenyekiti huyo wa IEBC akawaambia maseneta hao.

Bw Chebukati alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo kuelezea namna tume yake imejiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Huenda ni kutokana na marufuku kwenye sheria hiyo ambapo kiongozi wa ODM Raila Odinga ameandaa dhifa ya chakula cha jioni, na mchango kwa ajili ya kampeni zake za urais. Dhifa hiyo itafanyika katika hoteli ya kifahari ya Villa Rosa Kempinski, Nairobi ambapo washiriki watanunua sahani moja ya chakula kwa Sh1 milioni.

Itakumbukwa kwamba Rais Uhuru Kenyatta pia aliaandaa harambee kama hiyo katika mkahawa wa Safari Park Nairobi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017 ambapo zaidi ya Sh800 milioni zilichangwa ndani ya muda wa saa mbili.

Miongoni mwa waliohudhuria shughuli hiyo ni mabwanyenye ambao ni wanachama wa Wakfu wa Mlima Kenya (MKF).

Tangazo la IEBC la kuwazima wanasiasa kuchanga au kuchangiwa fedha ni pigo kwa wawaniaji ambao wanapania kuwania viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba wengi wao walikuwa tayari wameratibu shughuli mbalimbali za harambee hadi mwezi Aprili mwaka ujao, 2022.

Walipania kutumia majukwaa hayo kujipendekeza mbele ya wapigakura ili waweze kushinda katika kinyang’anyiro hicho.

Katika miaka ya nyuma, uwezo wa wawaniaji umekadiriwa kwa misingi ya jinsi wanavyoweza kuchangisha fedha kwa miradi mbalimbali ya umma, mwenendo ambao ulianza wakati wa enzi ya utawala wa rais wa pili nchini marehemu Daniel Arap Moi.

Wanasiasa hao wamekuwa wakitoa michango mikubwa kusaidia miradi ya makanisa, mazishi, harusi, makundi ya wahudumu wa bodaboda, akina mama wafanyabiashara, miongoni mwa makundi mengine ya kijamii.

Naibu Rais Dkt Ruto amekuwa akitoa michango ya mamilioni ya fedha makanisani, hali ambayo imemchangia Bw Odinga kumkosoa akidai pesa hizo ni za ufisadi.

You can share this post!

Real Madrid yakung’uta Bilbao na kufungua mwanya wa...

Kipchoge, Chepng’etich watoka bure tuzo ya mwanariadha...

T L