• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 6:55 PM
Wandani wa Ruto wamlima Rais Uhuru

Wandani wa Ruto wamlima Rais Uhuru

Na SHABAN MAKOKHA

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto sasa wamemwelekezea lawama Rais Uhuru Kenyatta wakidai anachochea ngome ya Mlima Kenya dhidi ya naibu wake ili kusambaratisha azma ya urais ya Bw Ruto, 2022.

Wandani hao kutoka Magharibi akiwemo aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa, Naibu Kiongozi wa United Democratic Alliance, Seth Panyako na seneta wa zamani Kakamega Bonny Khalwale, wamemgeukia Rais Kenyatta, wakimshutumu dhidi ya kutumia handisheki kati yake na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kumtatiza Bw Ruto.

Wakizungumza katika maeneo tofauti, watatu hao walimkashifu Rais Kenyatta kwa kutumia lugha ya mama alipokuwa akihutubia wafuasi wake Eneo la Kati wakidai anachochea Mlima Kenya dhidi ya Ruto.“Bw William Ruto alipomuunga mkono Raila Odinga mnamo 2007, hakuwa mwizi, alipomuunga Uhuru Kenyatta 2013 na 2017, hakuwa mwizi, lakini sasa anapotaka kuwa rais wanamwita mwizi na kuwaambia watu wamkatae.

Hii si vyema kwa Rais anayepaswa kuwa ishara ya umoja,” alisema Bw Echesa. Bw Echesa alimtaka Rais aseme ukweli na akane kwamba hawakuwa na muafaka wowote na Dkt Ruto, kuwa kila mmoja atatawala kwa miaka 10.

“Bw Kenyatta aliingia kwenye mkataba na Bw Ruto kwa misingi ya kirafiki na Ruto akaheshimu mkataba huo kwa kumuunga mkono Bw Kenyatta kupata urais 2013 na 2017. Sasa kwa kuwa anamaliza (Kenyatta) muhula wake wa miaka 10, ameamua kukiuka mkataba huo na kumgeuka Ruto.

Tunaomba sasa Mungu anayeishi amkomboe (Ruto) kupitia safari ya urais,”Bw Khalwale alimkashifu Rais kwa kumtishia naibu wake kwa kuwafurusha wafuasi wake kutoka kamati mbalimbali katika Bunge la Seneti na Bunge la Kitaifa, kuwaondoa maafisa wa General Service Unit kutoka ulinzi wa Ruto, na sasa anafanya kampeni kumpinga Ruto,” alisema.

Alimtaka Rais kujitokeza na kuwaeleza Wakenya ni nini hasa kilichosababisha mafarakano kati yake na naibu wake.“Tunataka kujua ni nini hasa Naibu Rais alimfanyia Rais Kenyatta ili kuruhusu haya,” alisema.

Bw Echesa akimtaka Rais Kenyatta kuheshimu afisi ya Naibu Rais. “Ili marafiki hao wawili wageukiane vibaya hivyo na kuanza kuanika uadui wao hadharani, ni sharti kuna kitu kibaya kilichotendeka kati yao. Kwa sababu sasa Rais Kenyatta ameamua kumtishia waziwazi Bw Ruto, tunataka atueleze ni kwa nini walitofautiana,” alidai Bw Khalwale.

Viongozi hao wakuu wamekuwa wakijibizana kwa matusi na vitisho katika kampeni zao kote nchini.Rais Kenyatta, anayempigia debe adui yake aliyegeuka kuwa rafiki, Bw Odinga, amekuwa akizuru ngome yake ya Mlima Kenya akifanyia kampeni azma ya urais ya Bw Odinga 2022.

Mnamo Oktoba 29, Kiongozi wa Taifa alipokuwa akihutubia wakazi mjini Ruiru, aliwaonya dhidi ya kumpigia kura mwizi atakayesambaratisha kazi aliyofanya.Aliwahimiza kumchagua kiongozi atakayewaleta Wakenya pamoja na kuboresha kazi iliyokamilishwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki na Rais Kenyatta.

Bw Panyako hata hivyo, amemtaka Rais kutekeleza ripoti ya Dung’u Lands Inquiry Commission na ile ya Tume ya Ukweli na Haki (TJRC), ikiwa hana doa.

You can share this post!

Kiunjuri avuna wawaniaji 20 wakiingia TSP

Tabasamu tele ufuo wa Pirates ukifunguliwa upya kwa umma

T L