• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 5:30 PM
Wanjigi sasa apata makao mapya Safina

Wanjigi sasa apata makao mapya Safina

NA JUSTUS OCHIENG

MFANYABIASHARA Jimi Wanjigi jana Jumatano alikihama rasmi chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na kujiunga na kile cha Safina anachopanga kutumia kuwania urais mwezi Agosti.

Bw Wanjigi aliyepokewa na Kiongozi wa chama hicho, Wakili Paul Muite ataidhinishwa na wajumbe kuwa mwaniaji wake wa urais wakati wa kongamano lililopangwa kufanyika Machi 21 katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

Hata hivyo, Bw Muite alisema endapo kutakuwa na mwanachama mwingine anayemezea mate tikiti ya kuwania urais kufikia siku hiyo, basi wajumbe watafanya uchaguzi ili kumpata mwaniaji bora.

“Kwa sasa ni Bw Wanjigi pekee ambaye ameonyesha nia ya kutaka ateuliwe na chama cha Safina kuwania urais. Wajumbe watakuwa na uhuru wa kumshirikisha kwenye mchujo endapo atajitokeza mwanachama mwingine,” akasema Bw Muite katika hoteli ya Serena, Nairobi.

Alimkabidhi Bw Wanjigi cheti cha kuwa mwanachama wa maisha wa Safina.

Aliwaaambia wanahabari kwamba chama cha Safina kitasimamisha wawaniaji katika nyadhifa zote, na kwamba hakitaingia kwenye makubaliano ya kuungana na yeyote kabla ya uchaguzi.

“Tunaenda peke yetu. Tutashirikiana tu na watu walio na fikira sawa na zetu baada ya uchaguzi mkuu ujao,” akasema Bw Muite.

Bw Wanjigi alisema kwamba alichukua hatua ya kujiunga na Safina baada ya ‘kufukuzwa kutoka ODM’.

“Tulikuwa ndani ya nyumba iitwayo ODM, chama ambacho nilijiunga nacho mwaka wa 2018 nikiamini kuwa sera na maono yake yalikuwa bora, baada ya kushirikiana na NASA mwaka wa 2017. Tulikuwa tumekuja pamoja kumaliza sera za ukandamizaji za serikali ya Jubilee. Lakini nilishangazwa na kiongozi wa chama changu kushikana mkono na Rais Kenyatta siku kama ya leo, miaka minne iliyopita,” akasema Bw Wanjigi.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Safina, John Wamagata, Duncan Nyale (mwenyekiti), mfanyabiashara Steve Mbogo na aliyekuwa mbunge wa Rangwe Martin Ogindo.

Bw Muite alisema Safina inaheshimu hadhi ya Wakenya akisema chama hicho kinapania kujenga taifa ambalo kila mwananchi anaweza kupata huduma za matibabu, nyumba bora na maji safi.

“Hiyo ndiyo kazi inayosalia kufanywa. Wanjigi aliamua kujiunga na Safina kutokana na itikadi na maoni yake kwa taifa hili,” akasema.

Bw Mbogo ambaye amekuwa mwanachama wa ODM alisema “tulijiunga na Safina kwa nguvu, bidii na matumaini ambayo hayajawahi kuonekana hapo awali.”

“Tunatumai kupata ukombozi wa kiuchumi kwa sababu panapo nia pana njia. Nchi hii inahitaji mkombozi. Imeathiriwa kiuchumi na hivyo inahitaji mkombozi wa kiuchumi.”

Bw Wamagata alikitaja chama cha Safina kama mrengo wa tatu ambao Wakenya wamekuwa wakisubiri kwa hamu na ghamu.

Bw Nyale alisema: “Tunatoa kauli mbiu kwa Wakenya. Tunakumbwa na changamoto ya kiuchumi na tuko tayari kutoa suluhisho; ingieni kwenye Safina ili muepuke dhoruba hii.”

“Nchini Kenya, Mkenya anahitaji nafasi ya kuishi maisha yenye thamani. Hakuna Mkenya ambaye anafaa kulala njaa kwa kukosa chakula.

“Tunataka kila Mkenya apate huduma za afya ambazo ni nafuu, nyumba za gharama ya chini, maji safi miongoni mwa mahitaji mengine muhimu.” akasema.

Bw Ogendo alimsifu Bw Wanjigi akimtaja kama mtu jasiri ambaye kila mara hulenga kuandikisha ufanisi katika kila jambo analofanya.

You can share this post!

Museo aghairi nia, sasa kutetea cheo chake uchaguzini

Anayedaiwa kubaka na kuiba apewa dhamana

T L