• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
Wapigakura wafafanulia wanasiasa matakwa yao

Wapigakura wafafanulia wanasiasa matakwa yao

NA KENYA NEWS AGENCY

WAPIGAKURA wanabadilisha mbinu kwa kutayarisha manifesto wanazoorodhesha masuala wanayotaka yapewe kipaumbele na viongozi wao.

Hii ni sehemu ya mdahalo unaoendelea ulioanzishwa na Inform Action and Network for Research and Governance (NRG), wa kutayarisha wapigakura wa wadi ya Sheywe, kaunti ya Kakamega ili wawachague viongozi wanaolenga kuwaletea maendeleo.

Kulingana na Mshirikishi wa shirika hilo la Inform Action eneo la Magharibi, Bi Winnie Wanjala, manifesto hizo za kijamii, zitawasilishwa kwa wawaniaji ambao watahitajika kuahidi kuzitekeleza kwa kutia saini.

“Tunaunganisha jamii ili zitoe mahitaji wanayotaka yapatiwe kipaumbele na kuyaweka katika stakabadhi na kisha watatia saini manifesto hizi wakiwa na viongozi wao. Viongozi wataahidi kwamba wakiingia mamlakani, watatekeleza miradi hiyo,” alieleza.

Alisema akiwa kijiji cha Maraba, wadi ya Sheywe kwamba kwa kawaida, wawaniaji wa viti tofauti vya kisiasa huwa wanatayarisha manifesto zao na kuzitoa kwa wapigakura, ambazo huwa hawatimizi wakichaguliwa.

“Kwa kawaida, ni wanasiasa wanaokuja na kutupatia manifesto, wakati huu, tunataka kufanya mambo tofauti eneo la Magharibi mwa Kenya,” alisema.

Shirika la Inform Action lilianza mpango huo Nyeri mwaka wa 2017, kwa kusaidia makundi ya wanawake kutayarisha manifesto ambazo waliwasilisha kwa viongozi wao.

Mmoja wa viongozi waliyempatia manifesto alichaguliwa, kisha akasaidia wanawake kuanzisha miradi ya uongezaji thamani kwa kutengeneza vibanzi kutoka kwa ndizi na kukuza maua ambayo yamekuwa yakiletea mapato wengi wao na kubuni nafasi za kazi.

“Kwa hivyo, mwaka huu tunasema ni wapigakura watakaotoa mahitaji wanayotaka yashughulikiwe na sio wanasiasa,” aliongeza.

Bi Wanjala alisema kwamba kutokana na hali ngumu ya uchumi na kupanda kwa gharama ya maisha, wakazi wanakabiliwa na presha na hali isiyotabirika, jambo linalohitaji viongozi kupigwa msasa ili kupata wale wanaojali na sio wafisadi.

Mashirika hayo mawili pia yanahimiza jamii kuchagua miradi muhimu kwa maisha yao ya kila siku.

“Pia tunakagua miradi ya zamani ya viongozi wetu ili kuona ikiwa walitimiza ahadi zao na iwapo walitumia vyema pesa za umma. Tunataka jamii kufanya hivi ili iweze kuchagua viongozi kwa kutegemea masuala wanayopatia kipaumbele katika jamii tofauti na si kuchapa siasa tu,” aliongeza.

Mkuu wa NRG kaunti ya Kakamega, Bw Paul Odongo alisema shughuli hizo zitafanywa katika wadi ya Sheywe kabla ya kupelekwa katika wadi zingine katika kaunti hiyo.

Alisema wakazi wametambua miradi itakayochunguzwa.

“Wapigakura wamelalamikia hali ya hospitali mbili za kiwango cha Level 2 au zahanati, mabomba ya maji taka, hali ya barabara na usalama,” aliongeza.

Alisema kwamba kamati ya watu tisa kutoka jamii ya eneo hilo itaundwa ambao watashirikiana na NRG na Inform action kuchunguza miradi.

Odongo alisema kutokana na mazungumzo na wakazi, wengi wao walisema wanataka kuchagua viongozi wanaowajibika tofauti na awali ambapo hawakujali aliyeingia uongozini.

You can share this post!

Mjakazi akiri kuiba mali ya mwajiri wake

Wakazi watofautiana na Rais kuhusiana na kutolewa hati za...

T L