• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Wazee warai Raila akubali baraka zao

Wazee warai Raila akubali baraka zao

Na GEORGE ODIWUOR

KUNDI moja la Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo, linamtaka kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga aende wabariki azma yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wazee hao walisema kwamba wakati umefika jamii ya Waluo imbariki mwana wao kwa kufanya tambiko la kitamaduni wakiongozwa na miungu anapoendelea na kampeni za kusaka urais wa nchi.

Mwenyekiti wa Baraza hilo Ker Nyandiko Ongadi na kiongozi wa baraza katika eneo la Karachuonyo Ager Kirowo walisema wanawakilisha msimamo wa jamii yao.

Bw Kirowo alisema wazee wameshauriana kuhusu suala hilo na wameamua kumwalikia kiongozi huyo wa ODM kwa mkutano ili waweze kumtawaza na kupata baraka kutoka kwa jamii.

“Tunamuomba kiongozi wa ODM kuja kwetu apate baraka. Tumekutana na viongozi wa kidini na makundi mengine na tukakubaliana kwamba hili linawezekana,” alisema.

Akizungumza akiwa Kendu Bay, Bw Kiriwo alisema eneo la hafla hiyo pia limetambuliwa na kundi lake linachosubiri ni jibu kutoka kwa Bw Odinga.

Ikiwa Bw Odinga atakubali ombi hilo, sherehe ya kumbariki itakuwa katika Alau Rachuonyo, uwanja wa kihistoria ulioko Kendu Bay ambako maamuzi muhimu ya kisiasa huwa yanafanyiwa.

Karachuonyo inajulikana kama nyumbani kwa viongozi wa zamani wa baraza hilo. Waliokuwa maafisa wa baraza hilo la wazee ni pamoja na Paul Mboya, Koyo Opien na Riaga Ogallo.

Bw Kirowo alisema kwamba wazee hao wanahisi wametengwa wakati wazee kutoka jamii zingine wameruhusiwa kumtawaza waziri mkuu huyo wa zamani anapotafuta uungwaji mkono kutoka maeneo yote ya nchi.

“Tuko na damu moja naye (Raila) kwa kuwa sisi ni wa uzao wa Ramogi. Tunamuomba aje ili tuweze kumpatia nguvu za kushinda wanaoshindana naye,” alisema.

Mnamo Septemba mwaka jana, mfanyabiashara Jimi Wanjigi alitembea nyumbani kwa Opiyo Otondi anayeongoza kundi jingine la Baraza la Wazee wa jamii ya Waluo kaunti ya Siaya kutafuta baraka zake na za jamii hiyo katika azima yake ya kugombea urais.

Bw Odinga pia ametawazwa na wazee wa jamii zingine zikiwemo Maa na Kuria ambao wameidhinisha azima yake ya urais.

Bw Nyandiko alisema kwamba aliamua kumbariki Bw Odinga baada yake kutangaza atagombea urais kwa mara ya tano.

“Tofauti na kiwango cha kitaifa, siasa za eneo hili zimevutia watu wengi na wapigakura hawajajua chama kitateua nani. Viongozi wakome kuchanganya watu,” alisema.

Bw Nyandiko aliomba watu kutoka eneo la Nyanza, ngome ya Bw Odinga kujisajili kwa wingi ili kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao.

  • Tags

You can share this post!

Mwalimu ashtakiwa kuwa na picha za ngono za watoto katika...

Oparanya aeleza kwa nini aliachia Raila nafasi

T L