• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Wiper iliteua Sonko naibu wa Mbogo – wakili aeleza

Wiper iliteua Sonko naibu wa Mbogo – wakili aeleza

NA PHILIP MUYANGA

CHAMA cha Wiper kilipenana barua kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kumteua mbunge wa Kisauni Ali Mbogo kama mgombea wake wa kiti cha ugavana Mombasa, mahakama kuu iliambiwa Jumanne.

Kupitia wakili Edwin Mukele, IEBC pia iliiambia mahakama kuwa kulingana na barua hiyo, Bw Sonko alikuwa awe naibu wa Bw Mbogo.

Bw Mukele alikuwa akiliambia jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo baada ya kuonekana kutofurahishwa na maamuzi yake (mahakama), mojawapo ikiwa hatua ya kuzuia kwa muda IEBC kuchapisha katika gazeti rasmi la serikali wagombeaji kiti cha ugavana kaunti ya Mombasa.

“Barua hiyo iko katika hati yetu ya kiapo,” Bw Mukele aliliambia jopo la majaji hao likiongozwa na Jaji Olga Sewe, Stephen Githinji na Anne Ong’injo.

Kulingana na hati ya kiapo ya afisa mkuu wa IEBC kaunti ya Mombasa Swalha Ibrahim, chama cha Wiper kiliandikia tume hiyo barua katika jaribio la kutekeleza uamuzi wa kamati ya tume hiyo ya kutatua mizozo (DRC).

Kamati hiyo ilitupilia mbali malalamishi ya Bw Sonko aliyekuwa akipinga kutoidhinishwa kugombania kiti cha ugavana na ikakipatia chama cha Wiper saa 72 kuteua mgombeaji mwingine.

“Barua hiyo iliwasilishwa kwa IEBC pamoja na cheti cha uteuzi cha Bw Ali Mbogo na Bw Sonko,” Bi Ibrahim alisema katika hati yake ya kiapo.

Bw Mukele pia aliiambia mahakama ya kuwa IEBC ilikuwa tayari imepeleka orodha ya wagombeaji ugavana wa Mombasa kwa mchapishaji wa serikali.

“Orodha ya majina ilipelekwa kwa mchapishaji wa serikali mnamo Juni 30 na ilikuwa ichapishwe mnamo Julai 1,” alisema Bw Mukele.

Hata hivyo,alizimwa na jopo hilo la majaji kuendelea kuongea baada ya kuashiria kuwa hakuna agizo lolote limetolewa nchini la kuzuia uchapishaji wa majina ya wagombeaji.

“Kama hakuridhishwa na maagizo basi unajua cha kufanya,” jaji Sewe alimwambia Bw Mukele.

Katika cheti chake cha kiapo, Bi Ibrahim pia alitaka mahakama kutupilia mbali kesi ya Bw Sonko akisema kuwa msingi wake ulikuwa ni makisio ambayo yalienda kinyume na ushahidi wake (Bw Sonko).

Bi Ibrahim pia alisema kuwa Bw Sonko alikuwa ameshindwa kuonyesha madai ya ukiukwaji wa haki zake.Mahakama pia ilikuwa imetoa maagizo ya kuzuia IEBC kutochapisha makaratasi ya kura kuhusiana na wagombea kiti wa ugavana kaunti ya Mombasa.

Pia, mahakama hiyo ilizuia chama cha Wiper kutomteua mgombeaji mwingine wa kiti cha ugavana katika kaunti ya Mombasa.

Maagizo hayo ya muda yalitolewa kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowekwa na Bw Sonko ambaye anataka uamuzi wa Bi Ibrahim na DRC wa kutomuidhinisha kugombania ugavana ufutiliwe mbali.

Mahakama kuu ilitarajiwa kutoa uamuzi wake siku ya Jumanne alasiri iwapo wakazi wawili wa Mombasa watajumuishwa katika kesi hiyo.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilitoa maelekezo kwamba kesi hiyo itaanza kusikilizwa leo Jumatano.

  • Tags

You can share this post!

Kabando adai ubaguzi ndani ya Azimio Nyeri

Mtetezi aomba KWS ipewe ufadhili zaidi

T L