• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Wiper yaahirisha mchujo kuruhusu maelewano

Wiper yaahirisha mchujo kuruhusu maelewano

Na PIUS MAUNDU

HATUA ya kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kubuni maelewano baina ya wawaniaji wanaowania nyadhifa mbalimbali kwa tikiti ya chama hicho, ilifanya shughuli za mchujo katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni kuahirishwa hadi Aprili 21.

Awali, chama hicho kilikuwa kimepanga kufanya shughuli hizo katika kaunti hizo tatu Jumanne wiki ijayo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bi Agatha Solitei, alisema kuwa hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa maelewano baina ya wawaniaji tofauti.

“Tuna mazungumzo mengi yanayoendelea kuhusu maelewano baina ya wawaniaji tofauti. Hilo ndilo limetufanya kuahirisha shughuli hizo katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni,” akasema Bi Solitei.

Kwa mara kadhaa, Bw Musyoka amesisitiza kuhusu haja ya wawaniaji kuwa na maelewano badala ya kushiriki mchujo.

Tayari amefaulu kumrai Bw Allan Sila kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha useneta wa Kitui, ili kumpa nafasi Seneta Enoch Wambua kutetea nafasi hiyo kwa tikiti ya Wiper kwenye uchaguzi wa Agosti.

Vilevile, chama hicho kimefanikisha maelewano kati ya Bi Priscilla Makumi na Mwakilishi wa Kike wa Kitui, Bi Irene Kasalu.

Bi Makumi alikuwa akilenga kuwania nafasi ya Uwakilishi wa Kike.

Badala yake, Bw Musyoka alimwahidi Bi Makumi uteuzi katika Bunge la Kaunti.

Kutokana na mafanikio hayo, Bw Musyoka ameongeza juhudi zake za kuwarai wawaniaji wanaolenga tikiti za Wiper kuwania ugavana katika kaunti za Kitui na Machakos kubuni maelewano baina yao.

Hapo jana, alikutana na aliyekuwa gavana wa Kitui, Dkt Julius Malombe na Bw Kiema Kilonzo, aliyehudumu kama balozi wa Kenya nchini Uganda.

Wawili hao wanalenga kupata tikiti ya Wiper kuwania ugavana katika kaunti hiyo.

Duru zilisema kuwa Bw Musyoka analenga kumrai Bw Kilonzo kujiondoa na badala yake kumuunga mkono Dkt Malombe.

Hata hivyo, Bw Kilonzo anasisitiza kuwa chama hicho kinafaa kuandaa shughuli za mchujo.

Kwa upande wake, Dkt Malombe anakitaka chama hicho kumpa tikiti ya moja kwa moja.

Kiongozi huyo anasisitiza kuwa itakuwa kupoteza fedha na wakati kuandaa shughuli ya mchujo kuamua atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi huo, akisisitiza kuwa Bw Kilonzo hana umaarufu hata kidogo.

Karata za kinyang’anyiro hicho zinaonekana kumchanganya sana Bw Musyoka, ikizingatiwa kuwa mwanawe, Bw Kevin Muasya, anapendekezwa kuwa mgombea-mwenza wa Bw Kilonzo.

Ni hali inayotajwa kuigawanya familia ya Bw Musyoka na chama cha Wiper kwa jumla.

Washirika wa Bw Musyoka ambao ni wapinzani wa Bw Kilonzo wanahofia kwamba ikiwa atashindwa, basi hilo litaathiri sana umaarufu wa Bw Musyoka kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Mchujo: Joho akosoa msimamo wa Shahbal

Wawaniaji wa kujitegemea wataka muungano wao usajiliwe

T L