• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 3:09 PM
Zani ajitosa katika ugavana wa Kwale

Zani ajitosa katika ugavana wa Kwale

NA SIAGO CECE

KINYANG’ANYIRO cha wadhifa wa ugavana kimeshika kasi baada ya Seneta Maalum, Bi Agnes Zani kutangaza azma yake ya kuwania kiti hicho.

Bi Zani ametangaza kuwa atagombea kiti hicho kupitia tiketi ya Orange Democratic Movement (ODM).

Kuingia kwake katika kinyang’anyiro hicho sasa kunavuruga mambo kwa Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, anayejitahidi kumrithi mkuu wake Salim Mvurya anayekamilisha hatamu yake ya mwisho.

Gavana Mvurya tayari amempendekeza Bi Achani kama mrithi wake ili aendeleze kazi aliyoanzisha.

Bi Zani na Bi Achani pia wanaonekana kama wagombea wakuu kutoka jamii ya Wadigo ambayo ni ya pili kwa ukubwa zaidi katika kaunti hiyo.

Wawili hao wanatazamiwa kushiriki kura kwa sababu wote wanaungwa na wakazi wengi.

Hata hivyo, wachanganuzi wanaamini Bi Achani yuko katika nafasi bora zaidi kuliko Bi Zani kwa sababu atajipigia debe kwa kutumia miradi ya maendeleo waliyoanzisha katika kaunti hiyo kuvutia wapigakura.

Anaonekana vilevile kuwa na uwezo zaidi kushinda wagombeaji wengineo kwa sababu ya uungwaji mkono anaofurahia kutoka kwa Gavana Mvurya, ambaye kwa sasa anadhibiti kura eneo hilo.

Wachanganuzi vivile wanasema kuwa Gavana Mvurya ana umaarufu mkubwa miongoni mwa wapigakura Kwale kutokana na kinachochukuliwa kama maendeleo aliyoyaleta kaunti hiyo, hivyo basi itakuwa rahisi kwa wapigakura kumchagua Bi Achani chini ya kivuli chake.

Akizungumza Kwale, Jumanne, Bi Zani alisema lengo lao la kuwa na zaidi

ya mgombea mmoja katika chama hicho ni kupigia debe ODM na kuhakikisha hawajitafutii kura wao peke yao bali pia kiongozi wa chama chao, Bw Raila Odinga.

“Nimeamua vilevile kuwa miongoni mwa wagonmbea wa wadhifa wa ugavana kwa sababu kuendeleleza ajenda ya ODM ambayo ni ngome katika kaunti yetu,” alifafanua.

Kiti cha ugavana Kwale kimevutia wagombea saba ambapo Bi Achani ana hakika ya kupata tiketi ya United Democratic Alliance (UDA) kuwania wadhifa huo. Bi Zani hata hivyo atalazimika kumenyana na wagombezi wengine watatu kwa tiketi ya ODM.

Wawaniaji hao ni pamoja na Spika wa Bunge la Kwale, Sammy Ruwa, Katibu wa Wizara aliyejiuzulu Prof Hamadi Boga na Mhandisi Chai Lung’anzi.

Alipokuwa akijiuzulu kama mtumishi wa umma mapema wiki hii, Profesa Boga alielezea imani kuwa ataibuka mshindi katika chaguzi za mchujo.

“Nina hakika nitashinda, Bw Lung’anzi ananiunga,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Jumuiya ya Afrika Mashariki iimarishwe...

Jitihada ni madini

T L