• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Michael Carrick kushikilia mikoba ya Man-United hadi kocha mrithi wa Solskjaer atakapoajiriwa

Michael Carrick kushikilia mikoba ya Man-United hadi kocha mrithi wa Solskjaer atakapoajiriwa

Na MASHIRIKA

BRENDAN Rodgers wa Leicester City, Mauricio Pochettino wa Paris Saint-Germain (PSG), Erik Ten Hag wa Ajax na kocha wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zdane ni miongoni mwa wakufunzi wanaohusishwa na uwezekano wa kupokezwa mikoba ya ukufunzi kambini mwa Manchester United.

Mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wanatafuta kocha mpya baada ya kuagana na Ole Gunnar Solskjaer aliyetimuliwa mnamo Jumapili, siku moja baada ya Man-United kupepetwa 4-1 na Watford ugani Vicarage Road.

Solskjaer alipigwa kalamu baada ya rekodi duni yaliyoshuhudia Man-United wakishinda mechi moja pekee kutokana na mechi saba za EPL. Matokeo hayo yaliwaweka miamba hao katika nafasi ya saba jedwalini kwa alama 17 huku pengo la pointi 12 likitamalaki kati yao na viongozi Chelsea.

Kuondoka kwa Solskjaer kulimpisha Michael Carrick ambaye sasa anashikilia mikoba ya Man-United wanaotafuta kocha atakayewaongoza hadi mwishoni mwa msimu huu wa 2021-22.

Solskjaer ambaye ni raia wa Norway, ni mchezaji wa zamani wa Man-United. Alichezea kikosi hicho kwa misimu 11 kati ya 1996 na 2007 na kukifungia mabao 126, likiwemo lililowavunia ushindi wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 1999.

Man-United sasa wanajiandaa kuvaana na Villarreal ya Uhispania kwenye UEFA mnamo Novemba 23, 2021 kabla ya vibarua vya EPL dhidi ya Chelsea na Arsenal mtawalia.

Darren Fletcher ambaye ni mkurugenzi wa kiufundi anasalia kambini mwa Man-United akisaidiwa kazi na Mike Phelan pamoja na Kieran McKenna waliokuwa sehemu ya benchi ya kiufundi iliyoongozwa na Solskjaer.

Solskjaer, 48, aliaminiwa fursa ya kushikilia mikoba ya Man-United mnamo Disemba 2018 baada ya kikosi hicho kuagana na kocha Jose Mourinho. Alipokezwa mkataba wa kudumu wa miaka mitatu mnamo Machi 2019 kabla ya kuurefusha kwa miaka mitatu zaidi hadi 2024 mnamo Julai, 2021.

Solskjaer ndiye kocha wa nne kudhibiti mikoba ya Man-United tangu Sir Alex Ferguson astaafu mnamo 2013. Ndiye aliyehudumu ugani Old Trafford kwa muda mrefu zaidi kuliko watangulizi wake David Moyes, Louis van Gaal na Mourinho.

Baada ya Man-United kukamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya pili mnamo 2020-21 kwa pointi 12 nyuma ya mabingwa Manchester City na kupoteza fainali ya Europa League dhidi ya Villarreal kupitia penalti, ilitarajiwa Solskjaer ashinde taji muhula hii ndipo ahifadhi kazi yake ugani Old Trafford.

Kufikia sasa, wanaselelea kileleni mwa kundi lao la UEFA baada ya mechi nne na wanajivunia alama sawa na nambari mbili Villarreal huku pointi mbili pekee zikiwatenganisha na nambari tatu Atalanta. Man-United tayari waliaga kivumbi cha Carabao Cup baada ya kudenguliwa na West Ham United ya kocha Moyes. Kikosi hicho bado hakijaanza kampeni za Kombe la FA muhula huu.

Baada ya kushinda mechi nne na kuambulia sare moja kutokana na mechi tano za ufunguzi wa kampeni za EPL msimu huu, Man-United walisuasua pakubwa huku wakizoa alama nne pekee kutokana na mechi saba zilizopita. Aidha, wamefungwa mabao 21 kutokana na mechi 12 ligini. Ni Norwich City na Newcastle United pekee wanaokamata nafasi mbili za mwisho jedwalini ndizo klabu ambazo zimefungwa mabao zaidi (27).

Kwa mujibu wa vyombo vingi vya habari nchini Uingereza, masogora wazoefu wa Man-United walipoteza imani na mbinu za Solskjaer ambaye kwa mujibu wao, asingeweza kushindana na wakufunzi Pep Guardiola wa Man-City, Jurgen Klopp wa Liverpool na Thomas Tuchel wa Chelsea.

Solskjaer anakuwa kocha wa sita wa EPL kupigwa kalamu msimu huu. Ni wakufunzi wanne pekee waliofutwa na klabu zao mnamo 2020-21 huku Slaven Bilic pekee akitimuliwa na West Bromwich Albion kabla ya Disemba 25, 2020.

Kufikia sasa msimu huu, Xisco Munoz wa Watford, Steve Bruce wa Newcastle, Nuno Espirito Santo wa Tottenham, Daniel Farke wa Norwich, Dean Smith wa Aston Villa na Solskjaer wa Man-United ndio ambao wamefutwa kazi na waajiri wao.

Man-United walitumia zaidi ya £110m mwishoni mwa msimu wa 2020-21 kusajili wanasoka Jadon Sancho (£73m), Raphael Varane (£34m) na Cristiano Ronaldo (£12.85m).

Chini ya kocha Solskjaer, Man-United walitumia zaidi ya £400m kusuka upya kikosi chao kwa kusajili Harry Maguire kutoka Leicester City kwa £80m, Aaron Wan-Bissaka kutoka Crystal Palace kwa £50m, Bruno Fernandes kutoka Sporting Lisbon kwa £47m na Donny van de Beek kutoka Ajax kwa £39m.

You can share this post!

Mahangaiko zaidi Miguna akijaribu kurejea nchini

Wakenya 4 waona giza tenisi ya Afrika ya Under-18 ikianza...

T L