• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
CHARLES WASONGA: Uamuzi wa Spika Wetang’ula kuhusu mrengo wa wengi bungeni una dosari

CHARLES WASONGA: Uamuzi wa Spika Wetang’ula kuhusu mrengo wa wengi bungeni una dosari

NA CHARLES WASONGA

UAMUZI wa Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Moses Wetang’ula, kuupa mrengo wa Kenya Kwanza (KKA) hadhi ya kuwa walio wengi una dosari na unaweza kubatilishwa kortini.

Sababu ni kwamba kupitia uamuzi huo, Bw Wetang’ula aliipokonya Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa mamlaka ya kuamua suala hilo kwa misingi ya mikataba iliyowasilishwa na KKA na Azimio la Umoja-One Kenya.

Spika huyo aliamua KKA ina jumla ya wabunge 179 huku Azimio ikiwa na 157; kwa sababu wabunge 14 waliochaguliwa kwa tiketi ya vyama vinne, ambavyo bado havijajiondoa rasmi kutoka Azimio, waliamua kujiunga na KKA.

Vyama hivyo vinne ni United Democratic Movement (UDM), Pamoja African Alliance (PAA), Maendeleo Chap Chap (MCC) na Movement for Democracy and Growth (MDG).

Bw Wetang’ula alidai wabunge hao 14 wamemwandikia barua wakidai kugura Azimio na kujiunga na KKA ya Rais William Ruto.

Lakini siku iyo hiyo Alhamisi wiki jana, Spika aliambia wabunge kwamba kulingana na rekodi zilizoko afisi ya msajili wa vyama, mrengo wa Azimio una wabunge 171 ilhali KKA ina 165.

Bw Wetang’ula alijikanganya mwenyewe alipodai kupokea barua ya wabunge 14 wa vyama vinne vya Azimio wakisema wamehamia KKA; lakini baadaye akasema vyama hivyo vimewasilisha kesi kortini vikitaka viruhusiwe kuondoka Azimio.

Inashangaza kuwa Spika aliamua wabunge hao wamehama Azimio, ilhali alitambua kwamba kesi zilizowasilishwa na vyama vyao kortini hazikuwa zimeamuliwa.

Izingatiwe UDM, PAA, MCC, na MDG viliwasilisha kesi kortini kwa sababu mkataba uliobuni muungano wa Azimio unaeleza kwamba, chama tanzu hakiwezi kuhama kabla ya miezi mitatu baada ya uchaguzi mkuu. Hii ina maana kuwa chama chochote kilicho ndani ya muungano kitaondoka tu baada ya Novemba 9, 2022.

Hii ina maana kuwa Bw Wetang’ula alifaa kuitambua Azimio kama mrengo wa walio wengi hadi wakati huo au baada ya kesi ambazo vyama hivyo vinne viliwasilisha kortini kusikilizwa na kuamuliwa.

Ilivyo sasa ni kwamba kufuatia uamuzi wa Spika huyo wa Bunge la Kitaifa, vyama vya UDM, PAA, MCC, MDG, na wabunge wao 14, ni wanachama wa miungano miwili; KKA na Azimio, kwa wakati mmoja.

Hili linakwenda kinyume na sehemu ya 10 ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa, 2022 na kipengele cha 108 cha Katiba.

Kwa hivyo, endapo Azimio itawasilisha kesi ya kupinga uamuzi huo wa Bw Wetang’ula, mahakama itabatilisha uamuzi huo kwa urahisi mno. Hii ni kwa sababu, awali, vyama vya PAA na MCC viliwasilisha kesi sawa na hiyo katika jopo la kutatua mizozo vya vyama (PPDT) na havikufaulu.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: NLC izilipe fidia familia ambazo ardhi...

Pep akiri Arsenal ni moto zaidi

T L