• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
AFC Leopards kuhamisha mechi zake za nyumbani kutoka Nyayo

AFC Leopards kuhamisha mechi zake za nyumbani kutoka Nyayo

NA JOHN ASHIHUNDU

AFC Leopards itahamisha mechi zake za nyumbani kutoka uwanja wa kitaifa wa Nyayo hadi Ulinzi Sports Complex unaopatikana kando ya barabara kuu ya Lang’ata kwenye Kaunti ya Nairobi.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dan Shikanda alisema wamelazimika kuchukua hatua hiyo kufuatia mpango wa Serikali kufunga viwanja vya Nyayo na MISC Kasarani ili vifanyiwe ukarabati kulingana na matakwa ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).

Mbali na viwanja hivyo vya Nairobi, kadhalika Serikali inatafuta mzabuni wa kurekebisha ule wa Kipchoge Keino Stadium unaopatikana katika Kaunti ya Uasin Gishu.

“Ingekuwa bora kama Shirikisho la Soka Nchini (FKF) lingeturuhusu kuchezea katika mojawapo wa Nyayo na Kasarani, wakati mmoja ukifanyiwa marekebisho, lakini iwapo haitawezekana, itabidi tupeleke mechi zetu Ulinzi Complex, ingawa hautatosha mashabiki wetu.”

Alisema huenda ukosefu wa viwanja vya kutosha ukavuruga mipango ya timu nyingi za (FKF-PL) zinazochezea mechi zao za nyumbani katika viwanja vya Kaunti hiyo.

Alisema, kwa mfano wakati wa mechi za ufungaji, Gor Mahia, Kariobangi Sharks, AFC Leopards, Nairobi City Stars, Posta Rangers zimepangiwa mechi kwa wakati mmoja, na huenda baadhi ya timu hizo zikalazimika kupeleka mechi zao William Ntimana Stadium mjini Narok au Kinoru Stadium, Meru.

Uwanja wa Ulinzi Sports Complex ulizinduliwa rasmi mnamo Aprili, 2022 na aliyekuwa rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na umekuwa ukitumiwa kuandaa mashindano mbali mbali ya vikosi vya jeshi, mbali na kutumiwa kuandaa mechi za FKF-PL.

Shikanda alisema Leopards wanakaribia kukamilisha usajaili wa wachezaji kadhaa wapya watakaosajiliwa kabla ya msimu mpya wa 2023/2024 kuanza Agosti 25.

Alisema timu yake inalenga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (FKF) baada ya kusubiri tangu 1998.

Kulingana na mwenyekiti huyo, lengo kuu ni kumaliza mabingwa wa ligi msimu ujao, jambo ambalo alisema litawezekana baada ya klabu hiyo kukubaliwa kusajili wapya baada ya marufuku ya FIFA kuondolewa mapema mwezi uliopita.

Leopards hawakuruhusiwa kusajili wachezaji kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita baada ya kustakiwa na wachezaji wa zamani wakiwemo Soter Kayumba, Bienvenue Shaka, Alex Kouassi, Gideon Waja na Vincent Habamahoro kutokana na deni.

“Muda wetu ofisini unamalizika 2026 na nitahakikisha kikosi iipo imara kuanzia rasmi msimu mpya baada ya wachezaji wapya kweka wino mikataba yao hivi karibuni. Kamwe sioni ugumu wa kutwaa ubingwa baada ya wachezaji wapya kuingia kikosini.”

Baada ya kuwapa matumaini makubwa mashabiki wao, Leopards walichanganyikiwa na hata kushindwa kumaliza msimu miongoni mwa tano bora, huku wakitosheka na nafasi ya saba jedwalini.

Katika mechi za maondoano za Mozzart Cup, Leopards walimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuichapa Ulinzi Stars 1-0 wikendi iliyopita, huku Kakamega Homeboyz wakitwaa ubingwa wa taji hilo baada ya kulaza Tusker 1-0 fainalini.

  • Tags

You can share this post!

Fahamu kwa nini unashauriwa kula nyama ‘halal’

Wandayi asema Raila yuko salama licha ya kutoonekana...

T L