• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Wandayi asema Raila yuko salama licha ya kutoonekana hadharani

Wandayi asema Raila yuko salama licha ya kutoonekana hadharani

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi amewahakikishia wafuasi wa Azimio la Umoja-One Kenya na Wakenya kwa ujumla kwamba kiongozi wa upinzani Raila Odinga yuko salama licha ya kutoonekana hadharani wakati wa maandamano dhidi ya serikali Jumatano na Alhamisi.

Akiongea na wanahabari Alhamisi, Julai 20, 2023, katika majengo ya bunge, Bw Wandayi alipuuzilia mbali uvumi kwamba Bw Odinga yuko mafichoni.

“Baba (Raila) yuko hai, buheri wa afya na mwenye uchangamfu mkubwa. Mkituona hapa mumemuona Baba. Maandamano yanayoendelea hayamhusu, yanawahusu Wakenya wote wanaoathirika na maisha magumu chini ya utawala dhalimu wa Kenya Kwanza,” akasema mbunge huyo wa Ugunja.

Bw Wandayi aliyeandamana na wabunge wanane wa Azimio alisema maandamano yanayoendelea sasa yamemilikiwa na wananchi wote bila kuzingatia miegemeo ya kisiasa na “hayahitaji uwepo wa Raila au kiongozi yeyote ili yafaulu.”

“Sote tunachangia katika juhudi hizi kwa hivyo wafuasi wetu hawafai kuingiwa na wasiwasi kuhusu kutoonekana kwa viongozi barabarani wakiongoza maandamano,” akaeleza Bw Wandayi.

Aliandamana na wabunge Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini), Samuel Atandi (Alego Usonga), Anthony Oluoch (Mathare) Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi na maseneta maalum Hamida Kibwana na Betty Syengo.

Bw Odinga hakuonekana hadharani Jumatano, Aprili 19, 2023 wakati wa siku ya kwanza ya wimbi la tatu la maandamano yaliyoitishwa na Azimio kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha na Sheria ya Fedha ya 2023 inayopendekeza nyongeza ya ushuru kwa bidhaa za kimsingi.

Lakini kwenye video zilizowekwa katika akaunti yake ya Twitter mnamo Alhamisi Bw Odinga alinakili visa ambapo polisi walitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji maeneo mbalimbali nchini Jumatano.

Jumla ya watu sita walipoteza maisha yao katika makabiliano hayo huku wengine wengi wakipata majeraha ya risasi.

Bw Odinga aliisuta serikali kwa kuruhusu maafisa wa polisi kuwaua waandamanaji kwa risasi licha ya kwamba watu hao hawakuwa na silaha zozote.

Hata hivyo, kinara huyo wa Azimio alisema kuwa maandamano hayo yataendelea Alhamisi na Ijumaa jinsi ilivyopangwa.

“Sauti ya umma sharti isikike. Maandamano yetu ya amani yataendelea,” Bw Odinga akasema kupitia Twitter.

Mara ya mwisho kwa Bw Odinga kuonekana hadharani ilikuwa ni Ijumaa, Julai 14, 2023, alipohutubia wanahabari katika Afisi za Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga (JOOF) katika mtaa wa Upper Hill, Nairobi.

Aliandamana na vinara wengine wa Azimio kama vile, Martha Karua, Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, Jeremiah Kioni, miongoni mwa wengine.

Wakati huo huo, Bw Wandayi ameshutumu kukamatwa kwa wabunge na wafuasi wengine wa Azimio siku ya Jumatano akisema kuwa hatua hiyo inakiuka Katiba na sheria husika.

“Hakukuwa na sababu maalum ya kukamatwa kwa waheshimwa Babu Owino (Mbunge wa Embakasi Mashariki), Ken Chonga (Kilifi Kusini) na Spika wa Bunge la Kilifi Teddy Mwambire kwa sababu hawakufanya kosa lolote. Kukamatwa kwa waheshimiwa hawa, mlinzi wa Raila Odinga ambaye ni Maurice Ogeta na msemaji wake Dennis Onyango hakufai kabisa,” akasema.

Mbunge huyo alisema kukamatwa kwa wafuasi hao wa Azimio hakutawavunja moyo wafuasi wa muungano huo ambao wamekuwa wakiandamana kupinga utawala dhalimu wa Kenya Kwanza.

Bw Wandayi na wenzake, pia waliilaani serikali kwa kile alidai ni kuamua kutumia magenge ya wahalifu waliopewa bunduki kwa ajili ya kuwaua waandamanaji.

“Kitendo kama hiki ni sawa na mauaji ya halaiki; aidha ni uhalifu wa kibinadamu wenye adhabu kali zaidi chini ya sheria za kimataifa,” akasema huku akitoa wito kwa Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) kufuatilia kwa “makini matukio nchini.”

Bw Oluoch alilaani hatua ya maafisa wa polisi kutumia njia za kikatili kupambana na waandamanaji katika mitaa ya Mathare na Kibra.

“Hawa watu waliojifanya kuwa polisi waliovalia kiraia kwa hakika ni wahalifu ambao walikodiwa na serikali kwa lengo la kuwaumiza na kuwaua watu wetu. Tunataka IPOA kuwachunguza watu hawa kwa sababu walinaswa vizuri katika picha za vyombo vya habari,” akasema mbunge huyo ambaye ni wakili.

Maseneta Syengo, Kibwana na Osotsi pia walilaani ukatili ambao polisi waliwatendea waandamanaji kote nchini.

“Polisi hawa wanafaa kufahamu kuwa hao watu ambao walikuwa wakiwaua kinyama ni raia wazalendo wa taifa hili ambao maisha yao pia yanalindwa chini ya Katiba ya sasa,” akasema Bi Kibwana.

  • Tags

You can share this post!

AFC Leopards kuhamisha mechi zake za nyumbani kutoka Nyayo

Wanawake waandamana kupinga agizo la kufungwa kwa saluni

T L