• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Nyanya, 71, akiri kuuza mihadarati Kasarani

Nyanya, 71, akiri kuuza mihadarati Kasarani

Na JOSEPH NDUNDA

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 71 aliyekamatwa akiuza chang’aa, bangi na tembe zinazoshukiwa kuwa mihadarati nyumbani kwake Kasarani, Nairobi, amekiri mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Bi Susan Wanjiru Kamau alipatikana na lita 50 cha chang’aa, misokoto 40 ya bangi na tembe zinazoshukiwa kuwa mihadarati katika nyumba yake katika kijiji cha Marurui.

Alikamatwa na polisi mnamo Septemba 22 baada ya chifu wa eneo hilo kudokezewa kuwa anauza vitu vilivyopigwa marufuku.

Chifu huyo aliongoza maafisa wa polisi kutoka kituo cha Marurui kuvamia makazi ya nyanya huyo ambapo bidhaa kadhaa zilikamatwa.

Ameshtakiwa kwa kosa la kulangua mihadarati. Aidha, alishtakiwa kwa kosa mbadala la kupatikana na mihadarati kinyume na sheria za nchi.

Alishtakiwa pia kupatikana na kinywaji cha pombe ambacho walisema hakikuafikia viwango vya ubora.

Mshukiwa alikiri mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu Monica Kivuti wa Mahakama ya Makadara na kuzuiliwa hadi Oktoba 6 ataposomewa maelezo ya kesi.

Chang’aa hiyo haikuwa imepakiwa kwenye chupa za mililita 250 kama inavyohitajika kisheria.

Tembe ambazo bado haijabainika ni mihadarati ipi zilizokuwa zimefichwa kwenye viatu ndani ya nyumba ya Bi Kamau zilinaswa na polisi walipata pia kilo moja ya majani ambayo wanashuku ni bangi.

Maafisa wawili wa polisi akiwemo inspekta wa polisi Pharis Ndungu ambaye aliongoza kikosi kilichomkamata Bi Kamau waliorodheshwa kama mashahidi katika kesi hiyo lakini hawatatoa ushahidi kufuatia kukubali mashtaka kwa mshtakiwa.

Nyanya hiyo atasalia rumande hadi Oktoba 6 akisubiri kuhukumiwa huku upande wa mashtaka ukisubiri matokeo ya ukaguzi wa tembe utolewe kama ushahidi.

  • Tags

You can share this post!

Wadau waambiwa utalii na usafi ni kitu kimoja

Tineja mshukiwa wa mauaji ya Eric Maigo kuzuiliwa kwa siku...

T L