• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Wadau waambiwa utalii na usafi ni kitu kimoja

Wadau waambiwa utalii na usafi ni kitu kimoja

NA KALUME KAZUNGU

WADAU wa Utalii, kaunti ya Lamu wamejitokeza kusafisha fuo za Bahari Hindi kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani.

Siku ya Utalii Duniani huadhimishwa tarehe 27 Septemba ya kila mwaka ambapo kila nchi mwanachama wa Shirika la Utalii Duniani husheherekea siku hiyo.

Wadau hao wakiongozwa na Waziri wa Utalii, kaunti ya Lamu, Aisha Abdallah Miraji, Mkurugenzi wa Utalii Lamu, Ali Ahmed, Afisa Mkuu Msimamizi wa Idara ya Utalii Joyce Murimi na wengineo walitekeleza usafi huo wa fuo za Bahari Hindi, hasa eneo la Wiyoni kisiwani Lamu na kutoa mwito kwa wenyeji, wageni na watalii kuyatunza mazingira ya ufukweni.

Bi Miraji alitaja usafi kuwa kigezo muhimu kinachofaa kuzingatiwa kwani watalii wengi huzuru maeneo ambayo ni nadhifu.

Alisema Idara ya Utalii kila mara imekuwa ikishirikiana na makundi mbalimbali ya kijamii, vijana, akina mama n ahata wanafunzi wa shule mbalimbali katika kuendeleza shughuli ya kusafisha mitaa na ufukwe wa bahari maeneo mbalimbali ya Lamu.

Bi Miraji alikiri kwamba utalii wa Lamu umekuwa ukifanya vyema siku za hivi karibuni kwani hoteli nyingi na mikahawa eneo hilo imejaa wageni, hasa msimu huu ambao ni wa watalii wengi wanaozuru eneo hilo.

“Tumejumuika na wanafunzi wa shule mbalimbali na vijana wanachama wa miungano mbalimbali kusafisha hizi fuo zetu. Kisiwa cha Lamu ni kivutio kikuu cha watalii na ni jambo mwafaka kuona kwamba usafi unazingatiwa ili kuwavutia watalii na wageni wengi hata zaidi,” akasema Bi Miraji.

Waziri huyo hata hivyo aliwashauri wakazi pia kuenzi tamaduni zao kama njia mojawapo ya kuwavutia watalii kuzuru eneo hilo.

“Mbali na usafi wa miji na fuo zetu, pia mimi ninazidi kuwasihi wakazi wa hapa Lamu kwamba tuenzi mila zetu ambazo kila mwaka ndizo zinazowavutia watalii kuja kujionea hapa, hasa wakati wa maadhimisha wa Tamasha za Utamaduni wa Lamu,” akasema Bi Miraji.

Aliishukuru serikali kuu kwa juhudi zake katika kudhibiti usalama wa eneo hilo, akisema licha ya changamoto zilizopo za kiusalama, Lamu bado inajivunia kurekodi idadi ya juu ya watalii na wageni wanaozuru eneo hilo.

Mwenyekiti wa Vijana wa muungano wa Safari Swimming and Entertainment Self-Help Group, Nasoor Mahfudh. Amewahimiza vijana kuzingatia usafi wa mazingira kuvutia watalii na kujipatia ajira. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Muungano wa Vijana wa Safari Swimming and Entertainment Self-Help Group, Nasoor Mahfudh aliwashauri vijana kujitolea kila wakati kutunza mazingira kwenye maeneo yao, akitaja kuwa ni kupitia mazingira safi, ambapo utalii utaimarika, hivyo vijana kujipatia ajira.

“Vijana wengi kama mimi hapa Lamu ni wahudumu wa matembezi ya watalii ufukweni. Ikiwa fuo zetu za bahaeri au miji yetu ni chafu, watalii watakwepa kuja hapa, hivyo kukosa ajira. Tuyatunze mazingiora yetu ili sekta ya utalii inoge, hivyo tujijengee ajira,” akasema Bw Mahfudh.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani mwaka huu ni ‘Utalii na Mbinu Jadidifu za Uwekezaji’ yaani ‘Tourism and Green Investments’.

Wakati wa Maadhimisho hayo ya Siku ya Utalii Duniani, wadau wa utalii, makundi ya vijana, akina mama na wanafunzi wa shule pia walipanda mikoko katika eneo hilo la Wiyoni.

  • Tags

You can share this post!

Madai wazazi wengi Rabai wanathamini matanga kuliko...

Nyanya, 71, akiri kuuza mihadarati Kasarani

T L