• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Bonge la mechi AC Milan dhidi ya Inter Milan nusu fainali UEFA

Bonge la mechi AC Milan dhidi ya Inter Milan nusu fainali UEFA

NA MASHIRIKA

MASHABIKI wanatarajia gozi la kukata na shoka ugani Stadio San Siro, Italia, wakati AC Milan na Inter Milan zitakabiliana mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), leo Jumatano usiku.

Ushindi kwa timu yoyote utawaweka guu moja mbele katika vita vya kunogesha fainali jijini Istanbul, Uturuki, mnamo Juni 10.

Pambano la leo lina msisimko wa kipekee kwani linakutanisha vigogo na mahasimu wawili wa jiji la Milan – Debi ya Milan.

Aidha, ni karibu miaka 20 tangu timu hizi mbili maarufu katika soka ya Italia zinogeshe nusu-fainali ya UEFA.

Wenyeji AC Milan – Milan kwa mashabiki wa soka – wanapigiwa upatu kutokana na historia yao pevu katika michuano hii.

Wametawazwa bingwa mara saba huku Real Madrid ikiwa ya pekee kubeba kombe hilo mara nyingi zaidi – 15.

Hata hivyo, mtihani wa leo sio rahisi ikikumbukwa kwamba majirani wao Inter Milan – Inter kama wanavyofahamika kwa mashabiki – wanajivunia washambuliaji hodari kwa sasa katika soka ya bara Ulaya.

Rafael Leao akitegemewa kuvuruga ngome ya Inter, Lautaro Martinez ataongoza mashambulizi dhidi ya Milan.

Leao ni miongoni mwa wa chezaji wanaong’ara kwa sasa baada ya kuchangia katika ushindi wa timu yake dhidi ya Waitaliano wenzao Napoli katika hatua ya robo-fainali.

Kwa upande wake, fowadi Martinez amekuwa katika kiwango kizuri tangu asaidie Inter kubwaga Benfica ya Ureno kwenye robo-fainali nyingine.

Mechi ya leo inatarajiwa kuwa na ushindani mkali ikizingatiwa timu zote zinalenga kuokoa msimu wao, baada ya kushindwa kuhimili mbio za kutwaa Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Napoli tayari wametwaa ubingwa wa Serie A muhula huu, baada ya ukame wa miaka 33.

Walifanikisha hilo katika sare ya 1-1 na Udinese mnamo Alhamisi iliyopita.

Kocha Simone Inzaghi wa Inter na mwenzake Stefano Pioli wa Milan wanafahamu fika kibarua kinachosubiri vikosi vyao leo usiku, na watatumai kila mchezaji atakuwa makini hadi mwisho.

AC Milan ilitwaa kombe la UEFA mara ya mwisho mnamo 2007, walipolipiza kisasi cha miaka miwili ya awali kwa kuibwaga Liverpool fainali iliyochezewa Istanbul.

Kadhalika, ni mara ya kwanza katika misimu 18 iliyopita kwa Milan kusakata 4-bora ya UEFA.

Isitoshe, nusu-fainali ya leo Jumatano ugani San Siro ni ya kwanza baina ya miamba hawa wa Italia katika miaka 20 iliyopita.

Milan walipenya kwa jumla ya bao 1-0 la ugenini wakati huo mnamo 2003, baada ya kuwa tisti sare tasa mkondo wa kwanza na 1-1 wa pili.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Serikali iandame wanaokwepa ushuru badala...

Umma kuruhusiwa kuuona mwili wa shujaa Mukami Kimathi

T L