• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Maajabu mashemeji wakicharaza baba ya mume

Maajabu mashemeji wakicharaza baba ya mume

NA TITUS OMINDE

MFANYABIASHARA mwenye umri wa miaka 60 mjini Eldoret amemshtaki mkwe wake pamoja na kaka zake wawili na baba yao kwa kumshambulia kabla kutoroka na binti mkwe wake.

Nyaraka za mahakama zinaonyesha kuwa mshtakiwa alimsababishia mlalamishi majeraha mwilini wakati wa tukio hilo.

Siku ya Jumatano Ibrahim Sadik, mwenye asili ya Kihindi, alisimulia Hakimu mwandamizi wa Eldoret, Mogire Onkoba jinsi wakwe zake walivyomshukia kwa kichapo cha mbwa katika boma lake mtaani Elgon -View.

“Nilipoteza fahamu kutokana na kipigo cha mbwa nilichokipata wakati wakwe zangu waliponishambulia kwa mateke na ngumi kutoka kila upande. Licha ya uzee wangu walinipiga bila huruma,” Bw Sadik aliambia mahakama huku akitoa ushahidi kuhusu tukio hilo.

Bw Sadik aliahidi kuwasilisha kortini kanda za video kutoka kwa kamera za siri, CCTV zikionyesha jinsi familia ya mshukiwa ilivyomlima kwa makonde, ngumi kwa mateke kutoka kila kona.

Sadik alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ambapo mkwewe Khalid Umar, kaka zake wawili Asif Salim na Tawqir Munir na baba yao Umar Mohammed kwa pamoja wanashtakiwa kwa kumpiga na kumjeruhi katika mtaa wa Elgon View mjini Eldoret Aprili 23, 2022.

Wanne hao wa familia moja wanakabiliwa na mashtaka ya kushambulia na kusababisha madhara halisi kinyume na kifungu cha 251 cha kanuni ya adhabu.

Pia walishtakiwa kwa shtaka mbadala la uharibifu wa mali ya mlalamishi.

Mlalamishi alijuta kuwa ilikuwa mwiko kwa mkwe kuwa na tabia za kugusana moja kwa moja na babake na mama mkwe kama mkwewe alivyofanya.

Pia alidai kuwa tukio hilo limemsababishia ‘mnyanyaso mkubwa wa kiakili’.

Kutokana na tukio hilo tayari mtoto wake ameanzisha mchakato wa kisheria wa talaka baada ya wakwe zake kutoweka na binti yao kwa nguvu kwenye ndoa yake pamoja na kumshambulia baba yake.

Washtakiwa walikanusha mashtaka hayo wakitaja madai ya baba yao mkwe wa zamani kuwa ni kinyume na mchakato wa talaka unaoendelea.

Waliachiliwa kwa dhamana ya Sh10, 000 pesa taslimu kila mmoja.

Mkwe anayehusika anatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo Juni 6 wakati itakapoendelea kusikilizwa.

  • Tags

You can share this post!

Sergio Busquets kuagana na Barcelona baada ya miaka 18...

Man-City pazuri kutinga fainali ya UEFA baada ya...

T L