• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Hit Squad kushiriki mashindano ya masumbwi DRC

Hit Squad kushiriki mashindano ya masumbwi DRC

CHARLES ONGADI

TIMU ya taifa ya Ndondi ‘Hit Squad’ itashiriki katika mashindano Afrika Zone 3 yatakayoandaliwa jijini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzia Machi 20-27.

Akizungumza na Taifa Leo Digitali, mkurugenzi wa mawasiliano wa Shirikisho la Ndondi Nchini (BFK) Duncun ‘ Sugar Ray ‘ Kuria amesema Kenya itawakilisha na kikosi kizima cha wanaume na wanawake walio kambini kwa sasa.

“Mabondia wetu wameiva kinyama baada ya kuwa katika kambi ya mazoezi kwa kipindi cha miezi minne,” akasema Kuria ambaye ni bondia wa zamani wa timu ya taifa.

Mara ya mwisho kikosi cha ‘Hit Squad ‘ kushiriki mashindano ya kimataifa ilikuwa ni mwezi Februari mwaka jana katika mashindano ya bara la Afrika kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki yaliyoandaliwa nchini Senegal.

Hata hivyo, mnamo Desemba mwaka jana Kenya ilipata mwaliko wa kushiriki mashindano ya kimataifa ya Bingwa wa Mabingwa nchini Tanzania lakini ikakosa kushiriki kutokana na msambao wa virusi vya Corona.

Aidha, kulingana na Kuria mara hii wana uhakika wa kushiriki mashindano haya ili kupima uwezo wa mabondia wa taifa kabla ya Michezo ya Olimpiki.

Hadi sasa ni mabondia wawili, Nick ‘ Commander ‘ Okoth anayezichapa katika uzito wa unyoya na Christine Ongare (fly) walio na uhakika wa kushiriki michezo ya Olimpiki ya Tokyo nchini Japan kuanzia mwezi Juni.

Kati ya mabondia wanaotarajiwa kutifua vumbi nchini DRC ni Elly Ajowi katika uzito wa Superheavy na Elizabeth Akinyi ambao wamepigiwa upatu kuchaguliwa na kamati ya kimataifa ya Olimpiki (IOC) kushiriki Michezo ya Olimpiki nchini Japan.

Kikosi cha ‘ Hit Squad ‘ kinaendeleza mazoezi yake makali katika ukumbi wa AV Fitness iliyoko eneo la Lavington Nairobi chini ya kocha Musa Benjamin.

Mataifa 12 yanatarajiwa kushiriki katika mashindano haya yatakayotumiwa pia kama kigezo cha kupima uwezo wa mabondia waliofuzu kabla ya mashindano ya Olimpiki.

You can share this post!

Hatuogopi mswada wa kumtimua Ruto serikalini – Kositany

Kupata chanjo hakumaanishi mlegeze masharti ya Covid-19 ...