• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Ronaldo awabeba Juventus dhidi ya Udinese katika Serie A

Ronaldo awabeba Juventus dhidi ya Udinese katika Serie A

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alifunga mabao mawili katika dakika za mwisho na kusaidia Juventus kuwapokeza Udinese kichapo cha 2-1 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Jumapili.

Chini ya kocha Andrea Pirlo, Juventus walijipata nyuma katika dakika ya 10 baada ya Udinese kufungiwa bao na Nahuel Molina. Hata hivyo, Ronaldo aliwarejesha waajiri wake mchezoni kupitia penalti ya dakika ya 83 kabla ya kuzamisha kabisa chombo cha wenyeji wao dakika sita baadaye.

Matokeo hayo yaliwapaisha Juventus hadi nafasi ya tatu kwenye msimao wa jedwali la Serie A kwa alama 69 sawa na AC Milan na nambari mbili Atalanta waliolazimishiwa sare ya 1-1 na Sassuolo. AC Milan ya kocha Stefano Pioli inakamata nafasi ya nne.

Inter Milan ambao tayari wamejizolea taji lao la kwanza la Serie A tangu msimu wa 2009-10, wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 82. Napoli wanafunga orodha ya tano-bora kwa alama 67, tatu zaidi kuliko Lazio waliosalia katika nafasi ya sita licha ya kuwakomoa Genoa 4-3.

Kufikia sasa, ni alama tano pekee ndizo zinatenganisha vikosi vinavyoshikilia nambari mbili hadi ya sita huku timu nne pekee za kwanza zikijikatia tiketi ya kushiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao wa 2021-22.

Juventus waliokuwa wakiwania taji la Serie A kwa mara ya 10 mfululizo msimu huu, sasa wangali na kibarua kigumu katika vita vya kuwania nafasi ya kukamilisha kampeni za muhula huu ndani ya mduara wa nne-bora na kujikatia tiketi ya UEFA.

Baada ya kupepetana na AC Milan katika mchuano wao ujao mnamo Mei 9, 2021 jijini Turin, Juventus watachuana na Sassuolo na Inter Milan kabla ya kumenyana na Atalanta katika fainali ya Coppa Italia mnamo Mei 19, 2021. Watafunga rasmi kampeni za Serie A msimu huu dhidi ya Bologna mnamo Mei 23, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Arsenal wacharaza Newcastle United 2-0 katika EPL

Miradi ya barabara na maji safi kuwafaa wakazi wa Kiambu